UNICEF: Ghasia za Haiti zasababisha watoto kuhama makazi
2 Julai 2024Kulingana na ripoti ya UNICEF, watoto waliokimbia makazi yao ni zaidi ya nusu ya jumla ya watu 600,000 ambao wamelazimika kukimbia makazi yao kutokana na ghasia, hasa katika mji mkuu wa Port-au-Prince ambao sehemu kubwa inadhibitiwa na magenge ya uhalifu.
Ripoti hiyo imedokeza kwamba idadi ya watoto waliokimbia makazi yao nchini Haiti imeongezeka kwa wastani wa asilimia 60 tangu mwezi Machi sawa na mtoto mmoja kwa kila dakika.
Mkurugenzi mtendaji wa UNICEF Catherine Russell amesema watoto nchini Haiti wanaendelea kustahimili mashambulizi ya hatari, ikiwa ni pamoja na ghasia za kutisha.
UNICEF imeonya pia ongezeko la vijana kujiunga na makundi yenye silaha ambayo yanaeneza ugaidi katika nchi ambayo asilimia 90 ya watu wanaishi katika umaskini, na watoto milioni tatu wanahitaji msaada wa kibinadamu.