UNICEF yasema mamia ya watoto wameuawa Syria
13 Machi 2017Kwa mujibu wa UNICEF katika ripoti yake iliyotolewa Jumatatu tarehe (13.03.2017) kiasi ya watoto 652 waliuawa katika mapigano nchini Syria mwaka 2016 ikiwa ni idadi kubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa na shirika hilo tangu lilipoanza kufuatilia mauaji kuhusiana na mgogoro huo.
UNICEF inasema idadi ya watoto waliotumikishwa kama askari katika mapigano hayo iliongezeka na kuwa zaidi ya watoto 850 ambayo inaonekana kuwa mara mbili zaidi ya ilivyo kuwa mwaka 2015.
Mkuu wa shirika hilo katika ukanda wa mashariki ya kati Geert Cappelaere amesema mateso yasiyo ya kawaida yameshuhudiwa katika kipindi hicho.
Baada ya miaka sita ya mapigano kiasi ya watoto milioni sita nchini Syria wanategemea misaada ya kiutu huku robo ya idadi ya watoto nchini humo wakiishi katika maeneo yaliyozingirwa na hivyo kuwa vigumu kufikiwa na huduma ya misaada ya kiutu na wengine wengi wanaishi katika maeneo ambayo ni vigumu kufikiwa kulingana na mazingira ya maeneo hayo.
UNICEF imesema watoto hawapotezi maisha eti tu kwa sababu ya mashambulizi ya risasi pamoja na mabomu lakini pia kwa sababu ya kukosa huduma ya madaktari na huduma nyingine za msingi ambapo pia mamilioni kadhaa ya watoto wamelazimika kuyahama makazi yao nchini Syria huku watoto milioni 2.3 wakilazimika kuvuka mipaka ya nchi hiyo na kwenda katika mataifa mengine ambako wanaishi kama wakimbizi.
Shule na hospitali zashambuliwa
Ripoti ya UNICEF inaonesha kuwa maeneo ya shule, hospitali, viwanja vya michezo na maeneo mengine ambayo hutumiwa na watoto yanazidi kutokuwa salama kutokana na kulengwa zaidi na mashambulizi ambapo UNICEF inasema kiasi ya watoto 255 waliuawa katika maeneo ya shule au jirani na maeneo hayo mwaka 2016.
Kutokana na kuongezeka kwa mateso yanayosababishwa na mgogoro huo baadhi ya familia zimefikia hatua ya kuwalazimisha watoto wao kuolewa au kutumikishwa katika ajira za watoto.
Mkuu wa shirika hilo katika ukanda wa mashariki ya kati anasema kila mtoto nchini Syria hivi sasa anaishi kwa wasiwasi kutokana na kutokuwa na uhakika juu ya majaliwa ya afya yake pamoja na hali ya baadaye ya maisha.
Mwandishi: Isaac Gamba/DPAE
Mhariri: Iddi Ssessanga