1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UNICEF: Vifo vya watoto vyapunguwa kwa nusu

13 Septemba 2013

Repoti ya Shirika la UNICEF imesema licha ya kwamba viwango vya vifo vya watoto duniani vimepunguzwa kwa nusu tokea mwaka 1990 takriban watoto 18,000 walio na umri usiozidi miaka mitano bado wanaendelea kufa kila siku.

https://p.dw.com/p/19h47
Mtoto wa Senegal.
Mtoto wa Senegal.Picha: AP

Ripoti iliyotolewa Ijumaa (13.09,2013) na Shirika hilo la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa UNICEF inaonyesha kwamba iwapo juhudi hazitoimarishwa dunia itashindwa kutimiza lengo la nne la Maendeleo ya Milenia la kupunguza kwa theluthi mbili kiwango cha vifo vya watoto vinavyoweza kuzuilika ifikapo mwaka 2015.

Kwa mujibu wa repoti hiyo ya UNICEF iliyotolewa kwa ushirikiano na Benki ya Dunia na Shirika la Afya Duniani (WHO)takriban watoto milioni 6.6 wamefariki kabla ya kutimiza miaka mitano hapo mwaka jana kulinganishwa na milioni 12 na laki sita waliofariki hapo mwaka 1990.

Ripoti hiyo imesema mafanikio hayo yametokana na watu kuweza kumudu matibabu na matibabu yenyewe kuwa na ufanisi, njia mpya za kutowa huduma za matibabu kwa watu maskini halikadhalika kuwepo kwa nia ya kisiasa kufanikisha jambo hilo.Hata hivyo repoti hiyo imesisitiza haja ya kuchukuliwa kwa hatua zaidi.

Mwenendo mzuri

Anthony Lake mkurugenzi mtendaji wa Shirika hilo la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF) amesema mwenendo huo ni mzuri na mamilioni ya maisha yameweza kuokolewa.

Watoto wakiwa furahani.
Watoto wakiwa furahani.Picha: UNICEF/SWIT2012-0002/Pirozzi

Ameongeza kusema hata hivyo vingi ya vifo hivyo vinaweza kuzuiliwa kwa kuchukuliwa hatua rahisi ambazo nchi nyingi tayari imezianzisha, kinachotajika ni kuliwekea suala hilo dharura kubwa zaidi.

Maeneo yote isipokuwa ya Oceania na eneo la kusini mwa jangwa la Sahara barani Afrika yameshuhudia kupunguka kwa vifo hivyo vya watoto kwa zaidi ya asilimia 50.Mashariki ya Asia vifo vya utotoni vimepunguwa kwa asilimia 74 na huko Afrika Kaskazini vifo hivyo vimepunguwa kwa asilimia 69.

Lakini kiwango cha vifo vya watoto bado ni kikubwa katika baadhi ya maeneo duniani ambapo vifo vya watoto walio na umri usiozidi miaka mitano bado vimetokea kwa takriban asilimia 80 hapo mwaka 2012 katika eneo la kusini mwa Jangwa la Sahara barani Afrika na Asia Kusini.

Watoto 18,000 hufariki kila siku

Hivi sasa takriban watoto 18,000 walio na umri wa chini ya miaka mitano hufariki kila siku.Nusu ya vifo hivyo hutokea katika nchi tano: China,Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo,India,Nigeria na Pakistan.

Mtoto akipatiwa chanjo ya polio Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.
Mtoto akipatiwa chanjo ya polio Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.Picha: picture-alliance/dpa

Afrika Magharibi na Afrika ya Kati ina kiwango kikubwa cha vifo vya watoto duniani walio na umri wa chini ya miaka mitano.Mtoto mmoja kati ya wanane walio na umri wa chini ya miaka mitano hufariki katika eneo hilo,kiwango ambacho ni kama theluthi moja ya watoto milioni 6.6 walio chini ya umri wa miaka mitano waliofariki duniani kote hapo mwaka 2012.

Sababu za vifo

Guido Borghese mshauri wa UNICEF wa kanda hiyo katika masuala ya kunusuru watoto na maendeleo ameliambia shirika la habari la Ujerumani dpa kwamba ni changamoto kwa mtoto kuzaliwa Afrika magharibi au Afrika ya Kati ambapo nafasi yake ya kuishi ni ndogo zaidi kuliko mahala pengine popote pale duniani.

Mtoto anayeuguwa malaria Afrika ya Kati.
Mtoto anayeuguwa malaria Afrika ya Kati.Picha: picture alliance/dpa

Sababu za vifo zinatajwa kuwa ni pamoja na homa ya mapafu, kuzaliwa kabla ya wakati, kukosa hewa ya kutosha wakati wa kuzaliwa,kuharisha na malaria.Asilimia 45 ya vifo hivyo inaweza kuhusishwa na ukosefu wa lishe ya kutosha.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP/dpa

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman