1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiSudan

UNICEF: Mamilioni ya watoto wapoteza makazi

6 Oktoba 2023

Shirika la UNICEF limeonya kuwa majanga yanayotokana na mabadiliko ya hali ya hewa kuanzia mafuriko, ukame, vimbunga hadi moto wa msituni yalisababisha watoto milioni 43.1 kupoteza makazi yao

https://p.dw.com/p/4XCM6
Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF, akizungumza wakati wa mahojiano na shirika la habari la Associated Press, mjini Kabul, Afghanistan, Ijumaa, Februari 25, 2022
Catherine Russell, Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEFPicha: Hussein Malla/AP Photo/picture alliance

 

Katika ripoti ya kina kuhusu suala hilo, shirika la UNICEF limeelezea visa vya kuhuzunisha vya baadhi ya watoto walioathiriwa, huku mtafiti mwenza wa ripoti hiyo Laura Healy akiliambia shirika la habari la Ufaransa AFP Kwamba takwimu zilizotolewa zilifichua tu sehemu ndogo ya tatizo hilo huku kukiwa na uwezekano mkubwa kwamba wengi zaidi waliathirika.

Watoto walioathirika waelezea masaibu yao

Khalid Abdul Azim, mtoto kutoka Sudan, ambaye kijiji chao kilikumbwa na mafuriko na kilikuwa kinaweza kufikika tu kwa kutumia boti, anasimulia kuwa walihamisha bidhaa walizokuwa nazo kwenye barabara kuu ambako waliishi kwa wiki moja.

Soma pia: Watoto milioni 4 wahitaji msaada wa kitu Pakistan - UNICEF

Mnamo mwaka wa 2017, Mia na Maia Bravo ambao ni ndugu walitazama moto ukiteketeza trela yao mjini California nchini Marekani kutoka nyuma ya gari dogo la familia. Katika ripoti hiyo, Maia anasema kuwa alipata mshtuko na kuanza kukosa usingizi usiku.

Takwimu hazizingatii umri wa waathiriwa

Takwimu za waliopoteza makazi yao ndani ya nchi zao kulikosababishwa na majanga ya hali ya hewa kwa ujumla hazizingatii umri wa waathiriwa. Lakini UNICEF ilifanya kazi na kituo kisicho cha kiserikali cha ufuatiliaji wa waliopoteza makazi yao ndani ili kufichua idadi ya watoto iliyofichwa.

Soma pia: UNICEF: Watoto takriban 100,000 wameathiriwa na tetemeko la ardhi Morocco

Ripoti hiyo inasema kuwa kati ya mwaka 2016 hadi  2021, aina hizo nne za majanga ya hali ya hewa ya ukame, vimbunga hadi moto wa msituni  ambayo kutokea kwake mara kwa mara kulisababishwa na ongezeko la joto duniani, kulisbabisha watoto milioni 43.1 kupoteza makazi katika mataifa 44.

Mafuriko yanayotokana na mvua kubwa katika eneo karibu na Kastamonu nchini Uturuki mnamo Agosti 11, 2021
Mafuriko yanayotokana na mvua kubwa katika eneo karibu na Kastamonu nchini UturukiPicha: DHA/AFP/Getty Images

Mafuriko na vimbunga vyasababisha hasara zaidi

Ripoti hiyo imeendelea kusema kuwa mafuriko na vimbunga vilisababisha kupotea kwa asilimia 95 ya makaazi. Healy, ameiambia AFP kwamba ilikadiriwa kuwa takriban watoto 20,000 walilazimika kuyahama makaazi yao kila siku na kusisitiza jinsi watoto walioathirika wanavyokuwa katika hatari ya kupata matatizo mengine kama vile kutengwa na wazazi wao au kukabiliwa na ulanguzi watoto. Takwimu hizo zinaonesha idadi ya watu waliopoteza makazi na sio idadi ya watoto walioathirika, kwasababu mtoto mmoja anaweza  kuhamishwa zaidi ya mara moja.

Soma pia:Hali mbaya ya hewa inasababisha pia maradhi kwa watoto na hata wazee kutokana na ongezeko la joto ama baridi kali

Takwimu hizo hazioneshi tofauti kati ya waliohamishwa kabla ya tukio la hali ya hewa, na wale waliolazimika kuyahama makazi yao kutokana na majanga. Kulingana na Healy, idadi ya watu waliopoteza makazi yao kutokana na ukame hairipotiwi kwa kiasi kikubwa, kwa sababu hautokei ghafla na hivyo kufanya vigumu kuhesabu.

Ripoti ya UNICEF yatoa utabiri

Ripoti hiyo ya UNICEF imetoa utabiri kiasi kwa baadhi ya matukio maalumu. Ripoti hiyo imetahadharisha kwamba katika miaka 30 ijayo, mafuriko yanaweza kusababisha watoto milioni 96 kupoteza makazi yao huku upepo unaotokana na kimbunga unaweza kuwalazimisha watu milioni 10.3 kuyahama makazi yao.  Mawimbi yanayotokana na  kimbunga yanaweza kusababisha watu milioni 7.2 kuyahama makazi yao. Kati ya makadirio hayo, hakuna yanayojumuisha uhamishaji wa kinga.

UNICEF imetoa wito kwa viongozi wa dunia kulishughulikia suala hilo wakati wa mkutano wa kilele wa hali ya hewa wa COP28 huko Dubai mnamo mwezi Novemba na Desemba.