UNICEF: Kizazi kijacho cha Yemen kimashakani
1 Februari 2019Katika barua iliyotumwa kwa Baraza hilo la Usalama, serikali hizo tatu zimewalaumu waasi wa Houthi kwa kukiuka makubaliano ya kusitisha mapigano katika mji muhimu wa bandari wa Hodeida mara 970 tangu yalipoanza kutekelezwa mnamo tarehe 18 Desemba.
Yemen, Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu umeliomba baraza hilo kuwashinikiza waasi hao na Iran inayowaunga mkono kuwa watachukuliwa hatua iwapo wataendelea kuyavunja makubaliano hayo yaliyofikiwa nchini Sweden miezi miwili iliyopita.
Shinikizo dhidi ya waasi wa Houthi
Waziri wa Umoja wa Falme za Kiarabu kuhusu masuala ya kigeni Anwar Gargash alikutana na Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres hapo jana kujadili changamoto za kuyatekeleza makubaliano hayo ya Stockholm.
Gargash aliwaambia waandishi wa habari kuwa wanaelewa kuwa wanahitaji kuwa na subira lakini lazima iwe na kikomo kwani hawataki kuanzisha tena mashambulizi dhidi ya Wahouthi bali wanachotaka ni Umoja wa Mataifa na jumuiya ya kimataifa kutumia nguvu zao kuhakikisha makubaliano yanayofikiwa yanaheshimiwa.
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilifanya kikao cha faragha kusikiliza ripoti kutoka kwa mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Yemen Martin Griffiths aliyekamilisha hivi karibuni duru nyingine ya ziara ya kidiplomasia kujaribu kuutatua mzozo huo.
Hayo yanakuja huku Mashirika ya kutoa misaada yakisema vita vya Yemen vimesababisha zaidi ya watoto laki tano kuyahama makazi yao katika kipindi cha miezi sita iliyopita, yakionya kuwa huenda Yemen ikawa na kizazi kilichopotea kutokana na mzozo unaoendelea.
Watoto milioni 2 hawapati elimu
Shirika la Umoja wa Mataifa linalowahudumia watoto UNICEF limesema watoto wengi waliyahama makazi ya kati ya mwezi Julai na Agosti mwaka jana kufuatia mapigano makali katika mji wa bandari wa Hodeida na sasa hawajui mustakabali wao wa siku za usoni utakuwaje kwani hawapati elimu, wanakumbwa na njaa na magonjwa.
Mkurugenzi wa UNICEF nchini Yemen Meritxell Relano amesema wanapoteza kizazi kwani watoto wengi hawasomi na kulazimika kuyahama makazi yao kunaifanya hali kuwa hata mbaya zaidi.
UNICEF imeonya kuwa watoto wasiopata elimu, hawataweza kupata ajira na kizazi ambacho hakijaelimika kitakuwa na maisha magumu katika siku za usoni.
Takriban watoto milioni 2 Yemen hawapati elimu baada ya vita vya takriban miaka minne ambavyo vimesababihsa vifo vya maelfu ya watu, mamilioni kuyahama makazi yao na mamilioni ya raia kukumbwa na baa kubwa la njaa.
Shirika la kutoa misaada kwa watoto la Save the Children limesema licha ya mapigano kusita kwa muda mjini Hodeidah, maelfu ya familia zinazidi kuutoroka mji huo zikihofia kuzuka upya kwa mapigano na raia hao wanahangaika kupata mahitaji ya kimsingi kama chakula, madawa na mafuta.
Mwandishi: Caro Robi/AFP/Thomson Reuters
Mhariri: Iddi Ssessanga