Watoto wanahitaji kusaidiwa kufikia malengo yao
23 Juni 2015Ripoti ya shirika hilo la kuwahudumia watoto la Umoja wa Mataifa, UNICEF inayoonesha kuhusu hali ya maendeleo ya watoto iliotolewa hapo jana usiku, imesema licha ya kuwa na mafanikio tangu viongozi wa dunia walipopitisha malengo ya millennia mwaka wa 2000, kutokuwepo haki sawa kwa watoto wote kumesababisha vijana wengi kufariki wakiwa wadogo au kuishi katika umasikini na kukosa elimu.
Mkurugenzi wa shirika hilo Anthony Lake, amesema malengo ya millennia yamesaidia kupatikana maendeleo makubwa, lakini pia yameonesha ni watoto wangapi wanaoachwa nyuma katika maendeleo hayo.
"Iwapo dunia itakubali hali ilivyo kuendelea tutawakatisha tamaa mamilioni ya watoto," alionya Anthony Lake.
Lakini katika habari nyengine ya kutia moyo ilioangaziwa katika ripoti hiyo ni kwamba, tangu mwaka wa 1990 vifo vya watoto chini ya miaka mitano vilishuka, idadi ya watoto wenye umri wa miaka chini ya 5 wanaokabiliwa na utapia mlo pia imepungua kwa asilimia 41 na mamilioni ya watoto wameweza kupata elimu ya msingi.
Kwengineko pia upande ambao sio wa kufurahisha, watoto milioni sita bado wanafariki kila mwaka kabla ya kutimiza umri wa miaka mitano na takriban watoto milioni 58 hawapati nafasi ya kwenda shule au kuanza elimu ya msingi.
Viongozi wa dunia wahimizwa kuchukua hatua za kuwasaidia watoto
Aidha Mkurugenzi Anthony Lake amewahimiza viongozi wa wa dunia watakaokutana baadaye mwezi wa Septemba kuwa na mpango mpya wa maendeleo 2030 kwa watoto waliopo katika mataifa masikini duniani, mipango ambayo wataikubali.
Ameongeza kuwa hatua hii itapunguza kiwango cha umasikini miongoni wa watoto wanaotokea familia za Kimaskini pamoja na ukosefu wa elimu hali inayoshuhudiwa kwa sasa.
Hata hivyo ripoti hiyo iliotolewa hapo jana imeonya kwamba kuendelea kushindwa kuwashughulikia watoto hawa kunaweza kuwa na matokeo mabaya sana.
Kwa sasa hali inayoendelea sasa shirika hilo la watoto la UNICEF limekadiria kwamba watoto zaidi ya milioni 68 walio chini ya miaka mitano watakufa kufuatia maradhi ambayo yanaweza kuepukika ifikapo mwaka 2030 na kwamba watoto miliono 119 watakabiliwa na utapia mlo ifikapo mwaka huo wa 2030.
Muandishi: Amina Abubakar/AP
Mhariri Yusuf Saumu