UN yatishia kusimamisha misaada ya kiutu Gaza
25 Oktoba 2023Tahadhari hiyo imejiri mnamo wakati msafara wa malori yaliyobeba misaada kama dawa, maji na vyakula vya Watoto ukivuka kivuko cha Rafah kutoka Misri kuelekea Gaza.
Hayo yakijiri, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amepinga kile alichokiita upotoshaji kutokana na matamshi yake jana mbele ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu shambulizi la Hamas.
Guterres amesema kauli yake haikumaanisha kwa vyoyvote vile kuhalalisha shambulizi la kigaidi la Hamas.
Soma pia:Maafisa wa Israel wamtaka Guterres ajiuzulu
Israel ilitangaza mzingiro kamili dhidi ya Gaza tangu shambulizi la kigaidi la Oktoba 7, lililofanywa na kundi la wanamgambo la Hamas ndani ya Israel na kuuawa watu 1,400.
Aidha kundi hilo la Hamas ambalo Israel, Marekani, Ujerumani na baadhi ya nchi zimeliorodhesha kuwa la kigaidi liliwashika watu 220 mateka na kuwapeleka Gaza.
Kulingana na takwimu za Hamas,idadi ya watu waliouawa Gaza kufuatia mashambulizi ya Israel ni zaidi ya 6,500.