UN yasema eneo la Darfur Kusini lapokea msaada wa chakula
20 Juni 2024Ujumbe wa WFP nchini Sudan umesema zaidi ya watu 50,000 wanakabiliwa na njaa kote Darfur Kusinihuku WFP ikijitahidi kuwafikishia msaada wa chakula kwa ushirikiano na shirika la misaada la World Vision.
WFP imesema sehemu nyingi za nchini Sudan, zimetumbukia kwenye mgogoro tangu mwezi April mwaka jana, yalipozuka mapigano makali kati ya jeshi la Sudan na kikosi cha wanamgambo cha RSF.
Soma pia: UN yaonya uwezekano wa janga la kibinadamu al Fashir
Mkuu wa masuala ya wakimbizi wa Umoja wa Mataifa Filippo Grandi, aliyehitimisha jana Jumatano ziara yake ya pili nchini Sudan tangu vita vilipoanza, ametahadharisha kwamba nchi hiyo inakaribia kutumbukia kwenye baa la njaa.
Naibu msemaji wa Umoja wa Mataifa Farhan Haq, amesema mvua kubwa zinazozotarajiwa hivi karibuni zinaweza kusababisha mafuriko makubwa ambayo yatazuia shughuli za kufikisha misaada.