UN yarefusha muda wa kikosi chake jimboni Abyei
12 Mei 2021Azimio hilo limekuja baada ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, kuliambia Baraza la Usalama kuhusu mkwamo wa mazungumzo kutokana na tofauti baina ya Sudan na Sudan Kusini. Jimbo la Abyei, lenye utajiri wa mafuta na ardhi yenye rutuba, linagombaniwa na nchi zote mbili ambazo zote zinadai kuwa eneo hilo linapaswa kuwa upande wake.
Mkataba wa mwaka 2005, uliopelekea uhuru wa Sudan Kusini mwaka 2011, unazitaka pande zote mbili kufikia makubaliano kuhusu adhi ya jimbo la Abyei, lakini suluhisho bado halijapatikana hadi sasa. Kikosi cha kulinda amani cha wanajeshi 3,700 wa Umoja wa Mataifa maarufu UNISFA, kilipelekwa huko Abyei tangu mwaka 2011.
Ratiba ya kuondolewa wanajeshi wa Umoja wa Mataifa
Azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limemuomba Katibu Mkuu Antonio Guterres kufanya mageuzi ya kimkakati kwa ajili ya kikosi cha UNISFA na kuwasilisha mapendekezo ya mageuzi hayo kwenye Baraza hilo ifikapo Septemba 30. Mageuzi hayo yanatakiwa kuyapa kipau mbele ulinzi na usalama wa raia wanaoishi jimboni Abyei.
Kwenye azimio la Novemba, Baraza la Usalama lilimuomba Guterres kuongoza mazungumzo ya pamoja baina ya Sudan, Sudan Kusini, Ethiopia na pande zingine husika katika mzozo huo ili kujadili mpango wa kuondoka kwa wanajeshi wa kikosi cha UNISFA.
Kwenye barua yake kwa baraza la Usalama, mwezi uliopita, Guterres alisema mazungumzo ya pamoja hayakuwezekana kutokana na janga la Covid-19, kwa hiyo alifanya mazungumzo tofauti na maafisa wa nchi tatu hizo.
Umoja wa Afrika kuingilia kati mzozo wa Abyei
Guterres alisema Sudan ilipendekeza kuondolewa kwa mpangilio kwa kikosi hicho mnamo kipindi cha mwaka mmoja. Lakini Sudan Kusini ilisisitiza umuhimu wa kuendelea kuwepo kwa kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa kutokana na wasiwasi wa kiusalama kwenye jimbo la Byei na Kordofan Magharibi.
Sudan Kusini ilitupilia mbali pendekezo la kuwepo na uongozi wa pamoja wa nchi mbili hizo kwenye jimbo la Abyei. Ikisema jaribio la aina hiyo lilisababisha kuzuka kwa vita mara mbili, kufuatia kutoaminiana kwa pande husika.
Kwa upande Ethiopia ilisema kuondolewa mapema kwa kikosi cha UNISFA kunaweza kuchangia hali kuwa mbaya zaidi kwenye jimbo hilo la Abyei.
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limezitaka Sudan na Sudan Kusini kuweka uongozi wa pamoja na makubaliano ya kiusalama kwa ajili ya Abyei. Huku likihimiza Umoja wa Afrika na mjumbe maalumu wa Umoja Mataifa kwenye eneo la Pembe ya Afrika kuendelea na juhudi za uingiliaji kati mzozo huo,ilikufikia maelewano kulingana na mkataba wa amani wa 2011.