UN yakosoa mswada unaowazuia wakimbizi kuingia Uingereza
8 Machi 2023Mswada uliozinduliwa leo huko Uingereza unaolenga kusitisha wahamiaji kuingia nchini humo kinyume cha sheria kwa boti ndogo ndogo, utasababisha marufuku ya kutafuta hifadhi. Haya yamesemwa na Umoja wa Mataifa ambao sasa unataka kutafutwe suluhisho lenye kuzingatia utu.
Shirika la kuwashughulikia wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR linasema lina hofu na mpango huo ambao utampa waziri wa mambo ya ndani wa Uingereza jukumu jipya la kisheria la kuwaondoa kutoka nchini humo wahamiaji wote wanaoingia kinyume cha sheria kama wale wanaoingia kupitia ujia wa Uingereza kwa kutumia mitumbwi kutoka Ufaransa.
UNHCR pia linasema mswada huo utawanyima ulinzi wanaotafuta hifadhi na ambao wanahitaji usalama na huenda pia wakawanyima kuwasilisha malalamiko yao, jambo ambalo litakuwa kinyume cha sheria za wakimibizi.