1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN yaishiwa fedha kuwahudumia wakimbizi wa Syria

6 Aprili 2013

Umoja wa Mataifa umeonya siku ya Ijumaa juu ya upungufu mkubwa wa ufadhili kwa wakimbizi wa Syria, ukisema kuwa mashirika ya misaada yanaweza kupunguza huduma kwa ongezeko kubwa la wakimbizi.

https://p.dw.com/p/18Arc
Kambi ya wakimbizi wa Syria ya Zaatari nchini Jordan.

Msemaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto la UNICEF, Marxie Mercado, amesema kwamba shirika hilo linafanya kazi kubwa lakini mahitaji yamezidi kuwa makubwa, na yanaongezeka kila siku, huku shirika hilo likiwa limeishiwa fedha. Mercado alisema shinikizo linaloendelea kutokana na ongezeko la wakimbikizi wanaofikia maelfu kila siku, linaongeza shinikizo kwa nchi ya Jordan.

Kamishna Mkuu wa shirika la wakimbizi la Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres.
Kamishna Mkuu wa shirika la wakimbizi la Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres.Picha: Reuters

Wakimbizi huenda wakakosa maji

Kutokana na kuishiwa fedha, UNICEF huenda ikalaazimika kusitisha utoaji wa huduma za maji kwa wakimbizi wa Syria nchini Jordan, ambako inasambaza karibu lita milioni 3.5 za maji ya kunywa kila siku kwa wakaazi karibu 100,000 wa kambi ya wakimbizi ya Zaatari. Mercado anakadiria kuwa idadi ya wakimbizi wa Syria nchini Jordan itafikia milioni 1.2 kufikia mwishoni mwa mwaka huu, idadi ambayo ni karibu moja ya tano ya wakaazi wa falme hiyo.

Kwa mujibu wa jeshi la Jordan, karibu Wasyria 1,750 walikimbilia nchini humo siku ya Ijumaa, na kuongeza idadi ya wakimbizi wapya waliowasili kufikia zaidi ya 15,000. Waziri Mkuu wa Jordan Abdullah Ensour alitangaza wiki iliyopita kuwa nchi yake imejipanga kuitangaza mikoa ya kaskazini kuwa eneo la janga kutokana na ongezeko la mfadhaiko unaowekwa na wakimbizi kwa rasilimali finyu za taifa hilo.

Wakati huo huo, kamati ya shirika la kimataifa la misaada la Red Cross ICRC imeonya juu ya madhara yatakayotokana na kupungua kwa misaada ya kibinaadamu kwa wasyria waliolaazimika kuyakimbia makaazi yao, katika nchi hiyo iliyoharibiwa na vita. "Ukosefu wa msaada wa kibinaadamu unaweza kuwa na madhara makubwa kwa maelfu ya watu nchini Syria," alisema Joroen Carrin, afisa wa ICRC anayehusika na shughuli za misaada nchini Syria.

Aliongeza kuwa wakimbizi wengi hivi sasa hawana kipato wala akiba, na wanategemea kwa kiwango kikubwa ukarimu wa wasyria wenzao na jamii ya kimataifa. Shirika la wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR limekadiria kuwa watu wasiopungua milioni 3.6 wameyakimbia makaazi yao nchini Syria tangu kuanza kwa uasi mwezi Machi mwaka 2011, dhidi ya rais Bashar al-Assad.

TO GO WITH AFP STORY BY MARIE ROUDANI Wakimbizi wa Syria wakiwa kambini katika eneo la Kherbet al-Khaldiye, mpakani mwa Syria na Uturuki.
Wakimbizi wa Syria wakiwa kambini katika eneo la Kherbet al-Khaldiye, mpakani mwa Syria na Uturuki.Picha: BULENT KILIC/AFP/Getty Images

Azidi kuinyooshea Uturuki kidole cha lawama

Al-Assad ameikosoa Uturuki, akiituhumu kwa kushiriki katika machafuko nchini Syria. "Serikali ya Erdogan imeshiriki kumwaga damu ya watu wa Syria," Al-Assad alinukuliwa akisema katika mahojiano na kituo cha televisheni cha Uturuki cha Ulusal, na gazeti la Aydinilik, yaliyorushwa siku ya Ijumaa. Aliongeza kuwa (Recep Tayyip) Erdogan hajasema neno moja la ukweli tangu kuanza kwa mgogoro huo, akimaanisha waziri mkuu wa Uturuki.

Uturuki imekuwa ikimsihi Assad ajiuzulu. Ofisi ya Assad ilisema mahojiano hayo yalifanyika mjini Damascus wiki hii, kufuatia taarifa kuwa alikuwa ameuawa. Waasi walisema siku ya Ijumaa kuwa waliteka kituo muhimu kutoka kwa wanajeshi wa serikali katika mji wa Um al-Mayathem karibu na mpaka na Jordan. Shirika la uangalizi wa haki za binaadamu nchini Syria lenye makao yake jijini London Uingereza, liliripoti kuwa waasi waliteka kituo cha kijeshi kilichopo katika barabara kuu kati ya Damascus na Jordan baada ya mapigano makali. Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, watu wasiopungua 70,000 wameuawa katika mgogoro wa Syria.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/dpae
Mhariri: Caro Robi