UN: Watu kadhaa wauawa katika mapigano katika eneo la Amhara
18 Novemba 2023Katika taarifa, msemaji wa ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa Seif Magango, amesema kuwa ni muhimu kwa pande zote katika mzozo huo kujiepusha na mashambulizi yasiyo halali na kuchukua hatua zote muhimu kulinda raia.
Magango ameelezea wasiwasi wake kuhusu athari mbaya za mashambulizi ya ndege zisizo na rubani na ghasia nyinginezo kwa wakazi katika eneo la Amhara huku kukiwa na mapigano yanayoendelea.
Soma pia:UN: Watu 183 wameuawa tangu mwezi Julai Amhara, Ethiopia
Magango ameliambia shirika la habari la AFP kwamba takriban watu 47 wameuawa katika mashambulizi matano tofauti tangu mwanzoni mwa mwezi Oktoba na kwamba wote walikuwa raia.
Katika hatua nyingine, waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken, ametoa tahadhari kuhusu ghasia hizo katika mazungumzo ya simu ya jana Ijumaa na waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed.
Msemaji wa wizara hiyo Matthew Miller, amesema kuwa Blinken alisisitiza umuhimu wa mazungumzo katika kutatua migogoro.