1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

UN: Takriban watu milioni moja watoroka makazi yao Gaza

16 Oktoba 2023

Shirika la Umoja wa Mataifa la kushughulikia wakimbizi wa Kipalestina mjini Gaza UNRWA limesema Jumapili kuwa takriban watu milioni moja wameyakimbia makazi yao katika siku saba za mwanzo za vita katika ukanda wa Gaza

https://p.dw.com/p/4XYg1
Shambulizi la anga la Israel katika ukanda wa Gaza mnamo Oktoba 15, 2023
Shambulizi la anga la Israel katika ukanda wa GazaPicha: Mohammed Fayq Abu Mostafa/REUTERS

Mkurugenzi wa mawasiliano wa shirika hilo la wakimbizi la UNRWA, Juliette Touma, ameliambia shirika la habari la AFP kwamba idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka kwa sababu watu wengi bado wanaendelea kuyahama makazi yao.

Israel inafanya mashambulizi ya kulipiza kisasi

Israel imekuwa ikishambulia ngome za kundi la Hamas katika ukanda huo wa Gaza baada ya kundi hilo kufanya mashambulizi makali ya kushtukiza Kusini mwa Israel mnamo Oktoba 7 na kuwauwa zaidi ya watu 1,300.

Soma pia: Maelfu wakimbilia kusini mwa Gaza kukwepa jeshi la Israel

Zaidi ya watu 2,300 pia wameuawa katika ukanda wa Gaza kutokana na mashambulizi ya anga ya Israel yanayowalenga viongozi wa Hamas,wanamgambo na maficho yao katika eneo la pwani .

Marekani, Umoja wa Ulaya, Ujerumani ikiwemo, pamoja na nchi nyingine kadhaa, zimeliweka kundi la Hamas kwenye orodha ya magaidi.