1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN: Muda wa kusitisha mapigano Aleppo hautoshi

Admin.WagnerD11 Agosti 2016

Umoja wa Mataifa umesema leo(11.08.2016) kwamba unajaribu kufanya mipango pamoja na Urusi kupata usitishaji mapigano unaowezekana wa hata masaa 48 katika mapigano yanayotokea katika mji uliogawika wa Aleppo.

https://p.dw.com/p/1JghA
Schweiz De Mistura in Genf
Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa Staffan de MisturaPicha: picture alliance/AP Photo/M. Trezzini

Umoja wa mataifa umeonya hata hivyo kwamba muda unakwenda mbio mno kwa watu takriban milioni mbili waliokwama katika mapigano.

Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Syria Staffan de Mistura alisema kwamba Urusi inatafakari kupanua usitishaji wa mapigano wa masaa matatu kila siku mjini Aleppo , na kusisitiza kwamba usitishaji wa masaa 48 unahitajika kuwezesha misaada kuwafikia wanaoihitaji.

Syrien Aleppo zerstörte Häuser und Tanklastzug
Eneo la mji wa Aleppo lililoharibiwa kwa vitaPicha: picture-alliance/Sputnik/M. Alaeddin

Urusi ilisema jana kwamba kutakuwa na usitishaji mapigano kila siku kwa masaa matatu mjini Aleppo kuanzia leo Alhamis, pendekezo ambalo mpatanishi wa Umoja wa mataifa alisema muda huo hautoshi.

Mshauri wa masuala la kiutu wa Umoja wa Mataifa Jan Egeland alisema kwamba usitishaji wa masaa 48 unahitajika kuhakikisha upelekaji salama wa misaada , na kuongeza kwamba ""kile ambacho ni kipya na chenye mwelekeo mzuri hivi leo ni kwamba Urusi imesema itataka kukaa chini na Umoja wa Mataifa pamoja na mwenyekiti mwenza mwingine Marekani kujadili vipi pendekezo hilo la Umoja wa mataifa litaweza kujadiliwa.

Syrien bei Aleppo Panzer der Opposition schießt
Kifaru cha jeshi la upinzani mjini AleppoPicha: Reuters/A. Ismail

Ongezeko la mapigano

Ongezeko la mapigano kuzunguka mji wa Aleppo limesababisha watu kadhaa kuuwawa katika muda wa wiki zilizopita, watu kadhaa wameyakimbia makaazi yao na karibu watu milioni mbili hawana maji wala umeme na pande zote mbili za mstari wa mbele wa mapambano , zimeathirika na kuporomoka kwa hali ya maisha kwa mamia kwa maelfu ya watu katika mji huo. Mkuu wa huduma za masuala ya kiutu wa Umoja wa mataifa Stephen O'Brien amesema.

Syrien Aleppo Krankenhaus Patient mit Atemmaske nach Giftgas Angriff
Mgonjwa katika hospitali mjini AleppoPicha: Reuters/A. Ismail

"Ndio sababu tutajadili na kwa kweli bila kubagua nchi yoyote mwanachama ambaye atatoa mapendekezo, lakini mwishowe , ni Umoja wa mataifa utabidi kusimamia upelekaji wa misaada kwa mujibu wa misingi iliyopo."

Katika vita hivyo ambavyo vimeingia katika mzozo wa kibinadamu, Umoja wa mataifa unasema mapigano hayo yanatishia kuongeza zaidi hali ya kuporomoka kwa huduma katika maeneo yale yanayodhibitiwa na waasi katika wilaya za mashariki za mji wa Aleppo kama miongoni mwa raia wanaoishi katika eneo la magharibi linalodhibitiwa na serikali.

Stephen OBrien PK UN
Stephen O'Brien akizungumza na waandishi habariPicha: Getty Images/AFP/L.Beshara

Wanaharakati nchini Syria wamesema mashambulizi ya anga yaliyolenga katika mji mkuu wa kundi la Dola la Kiislamu wa Raqqa yamewauwa leo kiasi watu 20 katika duru mpya ya mashambulizi ya anga ambayo yamekuja wakati Uturuki ikiitaka Urusi kufanya mashambulizi ya pamoja dhidi ya kundi la IS.

Mwandishi: Sekione Kitojo / ape / rtre

Mhariri: Caro Robi