UN: Mataifa yatekeleze vikwazo kuhusu Libya
16 Septemba 2020Azimio la Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa lilipitishwa siku ya Jumanne ambapo pia limezitaka nchi zote kuondowa mamluki wao walioko ndani ya nchi hiyo ya Afrika Kaskazini.
Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa pia limetowa mwito wa kufanyika mazungumzo ya kisiasa na kusitishwa mapigano katika nchi hiyo inayokabiliwa na vita vikubwa,huku likibaini kwa msisitizo kwamba hakuna suluhisho la kijeshi katika mgogoro huo.
Katika mchakato wa kulipigia kura azimio hilo kuhusu Libya wanachama 13 waliunga mkono na kuliidhinisha huku Urusi na China zikijizuia kupiga kura.
Kwa hivi sasa Libya toka kipindi cha miaka kadhaa baada ya kuangushwa madarakani na kuuwawa kiongozi wa muda mrefu wa nchi hiyo Muammar Ghaddafi, imetumbukia zaidi kwenye mgogoro na machafuko na imegawika vipande viwili, Mashariki na Magharibi, ambapo kila upande unaungwa mkono na makundi ya wapiganaji na wanamgambo wanaosaidiwa na nchi mbali mbali za kigeni zenye nguvu.
Kupitishwa azimio hili la baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kunafuatia ripoti ya hivi karibuni ya wataalamu wa Umoja wa Mataifa waliokuwa wakifuatilia kwa karibu utekelezaj wa vikwazo vilivyowekwa dhidi ya Libya.
Azimio hilo limeongeza muda wa ujumbe wa kisiasa wa Umoja wa Mataifa nchini Libya.
Ripoti ya wataalamu hao ilizishutumu pande zote mbili zinazopambana pamoja na washirika wao wa kimataifa wanaowaunga mkono,ambao ni Umoja wa Falme za Kiarabu, Urusi na Jordan kwa upande mmoja na upande wa pili ziko Uturuki na Qatar kwamba zinakiuka vikwazo hivyo vya silaha.
Aidha azimio la jumanne limeongeza muda wa ujumbe wa kisiasa wa Umoja wa Mataifa nchini Libya au UNSMIL hadi Septemba mwakani na kusisitiza juu ya dhima muhimu ya ujumbe huo katika kuratibu mchakato wa kisiasa wa Walibya wenyewe ukijumuisha pande zote katika kufikia lengo la kudumu la kusitisha vita.
Hivi sasa kazi ya mjumbe maalum wa zamani wa Umoja wa Mataifa Ghassan Salame aliyejiuzulu mwezi March imegawanywa vitengo viwili kama ilivyotaka Marekani.
Kitengo cha kwanza kikimjumuisha mjumbe maalum wa kusimamia UNSMIL kujikita zaidi juu ya mazungumzo na Walibya na upande wa wahusika wakimataifa ili kuumaliza mgogoro huo huku kukiwa na mratibu wa kusimamia operesheni za kila siku.
Katibu mkuu wa Umoja wa MataifaAntonio Guterres ametakiwa kwa mujibu wa azimio la baraza la usalama ateue mara moja atakayechukuwa nafasi ya mjumbe maalum Ghassan Salame.
Wanadiplomasia kadhaa wa Umoja wa Mataifa wamedokeza kwamba mwenye uwezekano wa kutwikwa jukumu hilo la mjumbe maalum ni mjumbe mwandamizi wa sasa kuhusu Mashariki ya kati Nickolai Mladenov ambaye aliwahi kuwa waziri wa mambo ya nje wa Bulgaria.
Ikumbukwe kwamba watalaamu wa Umoja wa Mataifa wanasema tangu Uturuki na Umoja wa Falme za Kiarabu zilipozidi kuingilia moja kwa moja vita vya Libya, uingizaji silaha katika nchi hiyo na mataifa hayo umeongezeka bila kujali vikwazo vilivyopo.
Uturuki ikiiunga mkono upande wa serikali juu mjini Tripoli wakati UAE ikiwa upande wa jenerali Khalifa Haftar anayetawala kivyake Mashariki ya Libya.
Soma Zaidi: Macron azikosoa Uturuki, Urusi mzozo wa Libya