1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN: Mamilioni wahitaji msaada wa kiutu Sahel

28 Aprili 2021

Umoja wa Mataifa na mashirika yasiyokuwa ya kiserikali yamesema watu milioni 29 wanahitaji msaada wa kibinadamu katika Ukanda wa Sahel kutokana na ukosefu wa usalama na njaa.

https://p.dw.com/p/3sg1H
Mauretanien Beduinen an Brunnen
Picha: Getty Images/AFP/A. Senna

Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayoratibu misaada ya kibinaadamu, OCHA na Baraza la Misaada kwa Wakimbizi la Norway, NRC pamoja na shirika la misaada la Plan International, imeeleza kuwa watu milioni tano zaidi watahitaji msaada na ulinzi kwa mwaka 2021 katika nchi za Burkina Faso, Cameroon, Chad, Mali, Niger na Nigeria, idadi hiyo ikiwa ni zaidi ya ile ya mwaka jana.

Nchi hizo sita kwenye eneo hilo la Afrika zimeharibiwa na vita. Mashirika hayo yamesema kuwa watu wameyakimbia makaazi yao kutokana na kukosekana kwa usalama na ghasia ambavyo vinatishia maisha, kuongeza ukiukaji wa haki za binaadamu na kuhatarisha mshikamano wa jamii.

Kukosekana kwa usalama pia kunazuia upatikanaji wa misaada ya kibinaadamu, hali inayoziacha jamii bila msaada muhimu na kuwaweka wafanyakazi wa mashirika ya misaada katika hatari zaidi.

COVID-19 yaifanya hali kuwa mbaya zaidi

Janga la virusi vya corona pia limeifanya hali kuwa mbaya zaidi katika eneo la Sahel. Watu wapatao milioni 5.3 hawana makaazi na maelfu ya shule zimefungwa na watoto milioni 1.6 wanakaridiwa kukumbwa na utapiamlo.

Chris Nikoi, Mkurugenzi Shirika la Mpango wa Chakula Duniani, WFP katika ukanda wa Sahel amesema wameshuhudia ongezeko la watu wanaokabiliwa na njaa, ikiwa ni takriban theluthi moja katika eneo la Afrika Magharibi idadi ya juu kabisa katika muongo mmoja. ''Kupanda wa bei ya vyakula kunakohusiana na ghasia pia kumesababisha njaa na utapiamlo, '' alifafanua Nikoi

Afrika Mali Unruhen Terror
Wanajeshi wa Mali wakiwa katika eneo lililoshambuliwa na kundi moja la waasi huko GaoPicha: AFP/Getty Images

Naye Mkurugenzi wa OCHA katika ukanda wa Sahel, Julie Belanger amesema nyuma ya takwimu hizo kuna hadithi za mateso ya kibinaadamu. ''Bila ya rasilimali za kutosha, mzozo huo utazidi kuongezeka, utapunguza uthabiti wa jamii na kuwaweka mamilioni zaidi ya watoto, wanawake na wanaume katika hatari,'' alibainisha Belanger

Umoja wa Mataifa umesema licha ya kuzorota kwa usalama katika miaka ya hivi karibuni, hali ya watu wa Sahel imezidi kuwa mbaya kwa zaidi ya muongo mmoja uliopita. Kati ya mwaka 2015 na 2020 idadi ya mashambulizi iliongezeka Sahel ya Kati na kuzidi mara tatu katika bonde la Ziwa Chad.

Eneo kubwa la Sahel ambalo lina ukame limekumbwa na ghasia kwa miaka kadhaa. Wapiganaji wenye itikadi kali za Kiislamu walianzisha mashambulizi kaskazini mwa Mali mwaka 2012 na kuzidi nguvu ya mashambulizi yaliyofanywa na waasi wa kabila la Tuareg.

Ufaransa iliingilia kati kupambana na wapiganaji hao wa jihadi, lakini walitawanyika na kujikusanya tena na kuanzisha kampeni katikati ya Mali mwaka 2015 na kisha kuingia nchi jirani za Niger na Burkina Faso. Chad na nchi za Ukanda wa Sahel kaskazini mwa Cameroon na Nigeria pia zimekumbwa na mizozo ya wapiganaji wenye itikadi kali za Kiislamu.

(AFP, DPA)