Kuwarejesha Nyumbani wahamiaji wa Afghanistan kutaleta mzozo
7 Oktoba 2023Umoja wa Mataifa umetahadharisha leo kuwa kuwarejesha kwa nguvu raia wa Afghanistan kutoka Pakistan kunaweza kusababisha ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu, ikiwemo familia kutenganishwa na usafirishwaji wa watoto.
Tahadhari hiyo imetolewa baada ya hivi karibuni Pakistan kutangaza msako mkali, dhidi ya wahamiaji wanaoishi nchini humo kinyume cha sheria wakiwemo raia milioni 1.7 wa Afghanistan.
Soma zaidi: Je, Pakistan itawafukuza wakimbizi milioni 1.7 wa Afghanistan?
Wahamiaji hao wametakiwa kurejea makwao kabla ya Oktoba 31, ili kuepuka kukamatwa na kufukuzwa nchini humo. Hata hivyo serikali ya Pakistan imekanusha kuwalenga Waafghani na kusema kuwa inafanya msako huo dhidi ya watu wanaoishi nchini humo kinyume cha sheria bila kujali utaifa wao.
Mashirika ya Umoja wa Mataifa yamesema kuwa Afghanistan inapitia katika mgogoro mbaya wa kibinadamu pamoja na changamoto kadhaa hasa suala la haki za wanawake. Serikali ya Taliban imewapiga marufuku wanawake kusoma zaidi ya darasa la sita, kufanya baadhi ya kazi na kuonekana katika maeneo mengi ya hadhara.