Dunia yampinga Netanyahu kuuchukuwa Ukingo wa Magharibi
11 Septemba 2019Umoja wa Ulaya ulionya kuwa ahadi hiyo ya Netanyahu inahujumu fursa ya kupatikana amani kwenye eneo la Mashariki ya Kati.
"Sera ya ujenzi na utanuzi wa makaazi ya walowezi ni haramu chini ya sheria za kimataifa na uendelezaji wake na vitendo vyote chini ya muktadha huu vinahujumu uwezekano wa suluhisho la mataifa mawili huru na matarajio ya amani ya kudumu." Lilisema tamko hilo lililotolewa mjini Brussels siku ya Jumatano (11 Septemba).
Saudi Arabia ilisema kuwa tamko hilo la Netanyahu ni batili kwa ujumla wake. Taarifa iliyotolewa na ufalme huo na kuchapishwa na shirika la habari la Saudi Arabia, SPA, ilisema kuwa "hatua hiyo ni uchokozi wa wazi dhidi ya Wapalestina na uvunjaji wa mkataba wa Umoja wa Mataifa na pia sheria za kimataifa."
Kauli kama hiyo ilitolewa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, ambaye alisema kuwa msimamo wa taasisi hiyo ya juu ulimwenguni kuhusu mzozo wa Israel na Palestina haujabadilika. Kupitia msemaji wake, Stéphane Dujarric, Katibu Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa alisema kwamba hatua yoyote ya upande mmoja haina manufaa kwa mchakato wa amani ya Mashariki ya Kati.
"Msimamo wetu haujabadilika na unaakisi maazimio ya Umoja wa Mataifa. Uamuzi wowote wa Israel kulazimisha sheria, mamlaka au utawala wake kwenye Ukingo wa Magharibi hauna uhalali wowote kwa sheria za kimataifa. Badala yake utazorotesha juhudi za mazungumzo, amani ya eneo hilo, na suluhisho la mataifa mawili huru," alisema Guterres.
Jumuiya ya Kiarabu yaonya
Mawaziri wa nje wa mataifa wanachama wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu walikutana kwa dharura hapo jana mjini Cairo, ambapo kwenye taarifa yao walisema kuwa tangazo hilo la Netanyahu linahujumu uwezekano wowote ule wa kufikiwa amani ya kudumu kati ya Waarabu na Israel, kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo, Ahmed Aboul Gheit, ambaye pia alisema kama likitekelezwa ni sawa na kutangaza mwisho wa mchakato wa amani.
"Jumuiya hii inalichukulia tangazo hili kama hatua mbaya na uchokozi mpya wa Israel kupitia dhamira yake ya kuvunja sheria zha kimataifa, Mkataba wa Umoja wa Mataifa na maazimio yake yanayohusika na uhalali wa kimataifa," alisema Aboul Gheit.
Tamko la Jumanne (10 Septemba) la Netanyahu lililenga kusaka kura za wapigakura wenye msimamo mkali, katika wakati ambapo mwanasiasa huyo mwenye utata akikabiliwa na upinzani mkali.
Kwenye mkutano huo, Netanyahu alisema ni lazima kwa Israel kuweka wazi muelekeo wake wakati Rais Donald Trump wa Marekani akijitayarisha kuzindua mpango wake wa amani ya Mashariki ya Kati.
Kuyachukuwa makaazi ya Bonde la Mto Jordan ambalo ni sawa na asilimia 30 ya Ukingo wa Magharibi kutaondosha kabisa matarajio ya kuundwa kwa dola la Kipalestina kandoni mwa Israel. Na kwenye hotuba yake hiyo, Netanyahu hakueleza nini anakusudia kuwafanya zaidi ya Wapalestina milioni mbili wanaoishi kwenye eneo analotaka kulichukuwa.