1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Ulaya yaiondolea Burundi vikwazo

21 Juni 2021

Mwakilishi wa Umoja wa Ulaya Claude Boshu, amebainisha kuwa msaada wa euro milioni 430 uliokuwa utolewe kwa kipindi cha 2015 hadi 2020 sasa utatolewa baada ya mazungumzo na Rais Ndayishimiye.

https://p.dw.com/p/3vINX
Burundi Präsident Evariste Ndayishimiye
Rais wa Burundi Evariste NdayishimiyePicha: Tchandrou Nitaga/AFP

Umoja wa Ulaya umechukuwa uamuzi wa kusimamisha vikwazo ilivyoiwekea Burundi tangu mwaka 2015. 

Mwakilishi wa umoja wa Ulaya, Claude Boshu, amebainisha kuwa msaada wa euro milioni 430 uliokuwa utolewe kwa kipindi cha 2015 hadi 2020 sasa utatolewa baada ya kupokelewa kwa mazungmzo na raia Evariste Ndayishimiye. Msemaji wa rais Ndayishimiye amesema rais ameikaribisha hatua hiyo. 

Baada tu ya kupokelewa kwa mazungumzo na rais Evariste Ndayishimiye, mwakilishi wa Umoja wa Ulaya nchini humu Claude Boshu amesema hatua ya kusimamishwa vikwazo imechukuliwa baada ya wataalam wa halmashauri mbali mbali za umoja huo kukutana na kuangazia hali ya Burundi.


"Kwa kauli moja wataalam kutoka nchi 27 za umoja wa ulaya wameagiza kuondolewa vikwazo vya kusimamisha misaada ya kifedha vilivyowekewa serikali ya Burundi, hii ni hatua kubwa na muhimu kwani miezi 6 hadi 7 iliyopita msimamo ulikuwa mwingine."

Mwanadiplomasia huyo wa Umoja wa Ulaya ameendelea kusema kuwa uamuzi huo ni kufuatia hatua za kuridhisha zilizoazimiwa na rais katika sekta za Utawala bora na kuheshimu haki za binaadam. Na kwamba kuna
matumaini ya kuwa katika miezi ijayo hatua nyingine zikaidhinishwa.

Soma zaidi: UN Walaani udhalilishaji wa wakimbizi wa Burundi

Kwa upande wake Evelyne Butoyi  msemaji wa rais amesema rais Ndayishimiye na muakilishi huyo wa Umoja wa Ulaya, wamekubaliana juu ya umuhimu wa kuwepo na mikakati imara ya serikali.


"Wamekaribisha ushirikiano ulivyo mzuri kati ya pande hizo mbili, hivyo wameagiza kuzidishwa kwa uwajibikaji kwa kubuni mikakati iliyo imara itakayoiruhusu Burundi kufikia maendeleo endelevu. Na kwamba dhamira ya ushirikiano huo ni kuboresha maisha ya raia."

Msaada wa fedha kwa serikali ya Burundi unaokadiriwa kufikia milioni 430 euro ulitarajiwa kutolewa tangu mwaka 2015 hadi 2020 lakini ulisimamishwa na umoja wa ulaya na kuitaka serikali kujadiliana na wapinzani walio uhamishoni.

Kigezo hicho kilitupiliwa mbali na  serikali ya Burundi, iliyowataja wapinzani hao kama wahusika wa jaribio la mapinduzi yaliyofeli mwaka 2015,  na hivyo kuchukuliwa hatua hiyo ya kusimamishwa misaada ya kifedha kwa serikali huku ikiendelea kutolewa misaada ya kiutu.

Tangu Febuari mwaka huu kumekuwa na majadiliano yanayo endelea kati ya serikali ya Burundi na Umoja wa Ulaya.

Umoja wa Ulaya ni mfadhili mkuu wa Burundi na kurudi kuisaidia kifedha serikali kutaipiga jeki kwenye bajeti ya serikali ambayo tangu kusimamishwa misaada hiyo imekuwa ikiendeshwa kutumia kodi na ushuru unaotolewa na raia.

Wakimbizi waishio Tanzania watakiwa kurejea Burundi