Umoja wa Ulaya watishia kuiwekea Georgia vikwazo
11 Desemba 2024Umoja wa Ulaya umetishia kuiwekea vikwazo serikali ya Georgia kufuatia machafuko na matumizi ya nguvu dhidi ya waandamanaji wanaoegemea upande wa Umoja huo wa Ulaya.
Msemaji wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya Kaja Kallas amesema hatua zinazoweza kuchukuliwa zitajadiliwa katika mkutano wa mawaziri wa Mambo ya Nje wa Umoja huo Jumatatu wiki ijayo.
Hata hivyo hakuweka wazi ni vikwazo vya aina gani vitakavyojadiliwa kwenye mkutano huo lakini pia amesema matumizi ya nguvu sio suluhisho la kuzima maandamano ya watu wanaodai kuona demokrasia na mustakabali wa Georgia katika Umoja wa Ulaya.
Hata hivyo Hungary imeshatishia kwamba itapinga hatua yoyote ya kupitishwa vikwazo dhidi ya Georgia.
Maandamano ya Georgia yamechochewa na uchaguzi wa bunge uliofanyika hivi karibuni,wanaodai ulikumbwa na dosari nyingi, na hatua ya chama tawala ya kutangaza kusitisha mazungumzo ya kutaka kuwa mwanachama wa Umoja wa Ulaya, hadi mwaka 2028.