EU yatarajiwa kuwawekea vikwazo maafisa wa Belarus
18 Agosti 2020Waziri wa mambo ya nje wa Uhispania Arancha Gonzalez Laya amekiambia kituo cha redio cha Onda Cero nchini mwake kwamba Umoja wa Ulaya unafikiria kuna nafasi ya kuweka vikwazo sio dhidi ya Belarus wala raia wake, bali dhidi ya watu waliochochea ghasia ama udanganyifu katika mchakato mzima wa uchaguzi.
Wakati huo huo balozi wa Belarus nchini Slovakia Igor Leshchenya ambaye amewaunga mkono waandamanaji wanaompingaAlexander Likashenko, kiongozi wa kiimla na wa muda mrefu wa Belarus, amesema leo kuwa amejiuzulu hii ikiwa hatua inayoashiria upinzani unaoongezeka katika ngazi za juu za serikali.
Wakati wa mahojiano na kituo cha habari cha Tut.by hii leo , Leshchenya alisema kuwa ni ''hatua ya busara'' baada ya kurekodi taarifa kupitia vidio kuunga mkono maandamano ambayo yamekuwa yakiendelea nchini Belarus kwa siku ya tisa mfululizo tangu kufanyika kwa uchaguzi wa urais Agosti 9 uliompa ushindi wa awamu ya sita Alexander Lukashenko. Leshchenya aliendelea kusema kuwa kama balozi ameteuliwa na rais na anatarajiwa kutekeleza sera zinazoamuliwa na yeye na kwamba wizara ya mambo ya nje nchini humo inaamini kuwa msimamo wake wa kiraia umekiuka matarajio hayo.
Lukashenko bado hajatia saini barua hiyo ya kujiuzulu kwa Leshchenya.
Hata hivyo wakati wa kongamano na wanahabari Lukashenko alisema kuwa hakuna mtu anayeweza kumwambiwa cha kufanyan na kwamba amekuwa uongozini kwa muda mrefu. Aliongeza kuwa hata katika wakati mbaya hatataabika na kwamba ni raia wa Belarus tu wanaoweza kumwambia cha kufanya.
Hapo jana viwanda kadhaa vikubwa vinavyomilikiwa na serikali vilitangaza migomo huku maelfu ya wafanyakazi wakiandamana kutaka kujiuzulu kwa Lukashenko. Rais huyo alisema jana kuwa huenda taifa hilo likaandaa uchaguzi mpya wa urais lakini hii inawezekana tu baada ya kuidhinishwa kwa katiba iliyofanyiwa marekebisho katika kura ya kitaifa ya maamuzi hizi zikiwa juhudi za kuchelewesha mambo huku mzozo wa kisiasa ukiongezeka.
Viongozi wa mataifa ya Magharibi wanasema kuwa uchaguzi huo haukuwa huru na wa haki na kuilaumu serikali ya nchi hiyo kwa msako wa ghasia dhidi ya waandamanaji. Hata hivyo rais wa baraza la Umoja wa Ulaya Charles Michel amesema kuwa mkutano wa dharura na viongozi wa Umoja huo utaandaliwa kesho Jumatano kuzungumzia uchaguzi huo na ukandamizaji dhidi ya waandamanaji.