1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Ulaya wakabidhiwa tuzo ya amani ya Nobel

Admin.WagnerD10 Desemba 2012

Umoja wa Ulaya umepokea tuzo ya amani ya Nobel leo mjini Oslo, ukitambuliwa na kamati ya tuzo hiyo, ambayo imetambua mchango wake wa kuendeleza utulivu na demokrasia.

https://p.dw.com/p/16zJc
Makabidhiano ya tuzo ya amani ya Nobel.
Makabidhiano ya tuzo ya amani ya Nobel.Picha: picture-alliance/dpa

Umoja huo umewatuma marais wake watatu katika sherehe hiyo ya mjini Oslo kupokea tuzo hiyo ya mwaka 2012, ambayo wakosoaji akiwemo mshindi wa zamani Desmond Tutu wanasema haukustahili. Lakini mwenyekiti wa kamati wa kamati ya Nobel, Thorbjorn Jagland amesema kamati yake haikukosea kuupa Umoja huo tuzo hiyo.

Mwenyekti wa kamati ya Nobel, Thorbjörrn Jagland.
Mwenyekti wa kamati ya Nobel, Thorbjörrn Jagland.Picha: Cornelius Poppe/AFP/Getty Images

"Umoja wa Ulaya umekuwa nguzo muhimu katika michakato hii ya maridhiano. Umoja wa Ulaya umesaidia kuleta udugu kati ya mataifa na kuendeleza mikutano ya amani ambayo Alfred Nobel aliiandika katika wosia wake. Kwa hiyo tuzo hii ya amani inastahili na ni muhimu, na sote tunatoa pongezi zetu," alisema Thorbjorn.

Wajigamba kuwa kinara wa kulinda amani

Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya, Herman Van Rompuy amesema tuzo hiyo ni ushahidi kwamba umoja huo ni chombo cha kulinda amani cha daraja la kwanza. Van Rompuy pamoja na rais wa halmashauri ya umoja huo Jose Manuel Barroso na rais wa bunge la umoja huo Martin Schulz wamekabidhiwa tuzo hiyo kwa pamoja.

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel na rais wa Ufaransa Francois Hollande ambao ni viongozi wenye ushawishi mkubwa katika kanda inayotumia sarafu ya euro, walikaa karibu wakati wa sherehe hiyo na walikuwa wakitabasamu na kunong'onezana mara kwa mara. Umoja wa Ulaya unakabiliwa na hali ngumu ya kiuchumi, kuongezeka kwa ukosefu wa ajira na mataifa kadhaa wanachama wa umoja huo hayawezi tena kulipa madeni yake.

Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya, Herman Van Rompuy.
Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya, Herman Van Rompuy.Picha: Cornelius Poppe/AFP/Getty Images

Maumivu hayo ya kiuchumi yamesababisha vurugu katika mataifa kadhaa, hususani Ugiriki ambayo inakabiliwa na kitisho cha kufilisika. Lakini kamati ya Nobel ilizingatia nafasi ya umoja wa Ulaya katika kuyaleta pamoja mataifa yaliyokuwa yanahasimiana katika bara hilo, muhimu zaidi ikiwa kuzibadilisha Ujerumani na Ufaransa kutoka maadui wakubwa na kuwa washirika wa karibu.

Kutoka mataifa 6 hadi 27

Kutoka mataifa sita tu yaliyokubali kuzalisha kwa pamoja nishati ya makaa ya mawe na chuma katika miaka ya 1950 na kufikia 27 leo hii, na 28 pindi Croatia itakapojiunga mwakani, Umoja wa Ulaya sasa unaanzia Ureno hadi Romania, na Finnland hadi Malta, na unatunga sheria na kanuni zinazoathiri zaidi ya watu milioni 500. Kamati ya Nobel ilisema mgawanyiko kati ya Ulaya mashariki na magharibi umepunguzwa kwa kiasi kikubwa, demokrasia imeimarishwa na migogoro mingi imesuluhishwa.

Rais wa Halmashauri ya Ulaya, Jose Manuel Barroso, amesema tuzo hiyo ni utambuzi wa mafanikio ya umoja wa Ulaya katika kipindi cha miaka 60, na pia kuuhamasisha umoja huo kwa ajili ya wakati ujao. Vijana wanne kutoka Ulaya akiwemo msichana mwenye umri wa miaka 12 kutoka Uhispania na mwanamke mwenye miaka 21 kutoka Poland nao walihudhuria sherehe hiyo baada ya kushinda mashindano. Viongozi 20 wa nchi na serikali za umoja huo pia walihudhuria.

Rais wa Halmashauri ya Ulaya, Jose Manuel Barroso.
Rais wa Halmashauri ya Ulaya, Jose Manuel Barroso.Picha: John MacdougalllAFP/Getty Images

Kiasi cha euro 930,000, sawa na dola za Marekani milioni 1.25 zinazotolewa sambamba na tuzo hiyo zitagawiwa kwa miradi inayosaidia watoto walioko katika maeneo yenye vita, ambapo wapokeaji watatangazwa mwakani. Umoja wa Ulaya umesema utajaliza fedha hizo za zawadi na kufanya jumla ya fedha zitakazotolewa kwa miradi itakayochaguliwa kuwa euro milioni mbili.

Uamuzi huo umewanyamanzisha wakosoaji katika mtandao wa Twitter na mitandao mingine ya kijamii ambao hapo awali walikuwa wakitania kwamba kama tuzo hiyo ni ya raia wote wa Ulaya, basi wote wanapaswa kugawana fedha za zawadi ambapo kila moja angepata euro 0.2.

Sauti zaidi zapinga Umoja wa Ulaya kupewa tuzo hiyo

Si watumiaji wa mtandao pekee wanaokosoa tuzo hiyo kutolewa kwa umoja huo, Desmond Tutu kiongozi wa Kanisa ambaye alipambana dhidi ya ubaguzi wa rangi katika nchi yake ya Afrika Kusini, alisema wiki iliyopita kuwa umoja huo haukustahili kupata tuzo hiyo. Siku ya Jumapili, karibu watu 1,000 wanachama wa vyama vya mrengo wa kushoto na makundi ya haki za binaadamu walianadamana katika mitaa ya jiji la Oslo wakisema Umoja wa Ulaya siyo mpokeaji anayestahili wa tuzo hiyo chini ya masharti ya Alfred Nobel aliyoyabainisha katika wosia wake mwaka 1895.

Kansela Angela Merkel (wa tatu kushoto) akishikana mikono na rais Francois Hollande wa Ufaransa (wa tatu kulia) wakati wa sherehe ya kukabidhi tuzo hiyo.
Kansela Angela Merkel (wa tatu kushoto) akishikana mikono na rais Francois Hollande wa Ufaransa (wa tatu kulia) wakati wa sherehe ya kukabidhi tuzo hiyo.Picha: Reuters

"Alfred Nobel alisema tuzo hiyo laazima itolewe kwa wale wanaofanya kazi kwa ajili ya kuondoa matumizi ya silaha," alisema Elsa-Britt Enger, mwenye umri wa miaka 70 ambaye anawakilisha shirika la 'Grandmothers for Peace' na kuongeza kuwa Umoja wa Ulaya haufanyi hivyo. Alisema umoja huo ndiyo moja ya watengenaji wakubwa wa silaha duniani.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/rtre
Mhariri: Josephat Nyiro Charo