Umoja wa Ulaya waburuza mataifa ya Afrika kutia saini mikataba ya EPA.
16 Desemba 2007Namibia imetia saini mkataba wa EPA , ambao ni mkataba baina ya mataifa ya umoja WA Ulaya na mataifa ya Afrika. Namibia ilitia saini mkataba huo hapo Desemba 12, lakini maafisa wa serikali ya nchi hiyo wanalalamika kuwa umoja wa Ulaya ulikuwa unatumia mbinu za kibabe kuzilazimisha nchi masikini kutia saini makubaliano hayo.
Tumesalimu amri, amelalamika mwanadiplomasia mmoja kutoka Namibia . Tumetia saini Desemba 12. Mbinyo ulikuwa mkubwa sana . Sekta ya binafsi ilikuwa inahisi kuwa wanaweza kupoteza soko na kujikuta wameathirika vibaya. Kwa upande wa masoko wangepoteza soko la nyama , matunda, samaki na bidhaa zitokanazo na samaki.
Nguvu za kisiasa na kiuchumi za umoja wa Ulaya pekee ni kitisho na mbinyo katika majadiliano, ameeleza mwanadiplomasia huyo bila kutaka kutajwa jina lake.
Wakati ukijadiliana na mshirika ambaye ana nguvu , unaishia kuburuzwa tu. Mbinu za ubabe zinatumika pamoja na vitisho, unaambiwa unatia saini ama unapoteza soko, ameongeza mwanadiplomasia huyo.
Hadi katika wakati wa mwisho, serikali ya Namibia ilijaribu kuzuwia mbinyo kutoka kwa sekta yake ya binafsi pamoja na umoja wa Ulaya.
Hadi mwishoni mwa juma lililopita , waziri wa biashara Immanuel Ngatjizeko alikuwa kimsingi amesema kuwa madai yaliyowekwa na mpango huo wa EPA kwa Namibia yalikuwa hayakubaliki.
Amesisitiza kuwa mkataba wa EPA ni lazima usaidie kuunganisha nchi za eneo na sio kuzigawa. Tumefanya makosa chungu nzima , mwanadiplomasia huyo ameliambia shirika la habari la IPS. Hakukuwa na uratibu sahihi miongoni mwa mataifa ya Afrika , Caribean na Pacific , ACP. Umoja wa Ulaya umefanikiwa kuyagawa mataifa ya ACP, sio tu kimkoa lakini hata ndani ya mikoa hiyo.
Jumuiya ya maendeleo ya kusini mwa Afrika SADC ina mataifa 15. Wakati mataifa hayo yalikuwa yakipata misaada ya maendeleo kutoka umoja wa Ulaya kwa jumla , hivi sasa ni nchi saba tu za SADC zile ambazo zimetia saini mkataba wa EPA ndizo zitapata misaada hiyo ya maendeleo ambayo inahusiana na EPA. Hii itakuwa na athari zake.
Umoja wa soko huria katika nchi za SADC unapaswa kuanza rasmi mwaka 2008. Ni vipi hali hii inaweza kufanyika , ikiwa baadhi ya nchi zimetia saini mikataba ya EPA wakati nchi kama Angola imeamua kutosaini mkataba wa EPA, hili bado halijapatiwa ufumbuzi.
Mwanadiplomasia huyo wa Namibia aliongeza haraka kuwa wakati nchi hiyo imetia saini mkataba huo hapo Desemba 12, imefanya hivyo huku ikitia shaka kuhusiana na baadhi ya vifungu. Iwapo shaka hii haitaweza kuondolewa katika awamu ijayo ya majadiliano , basi tunaweza kusema hatutakuwa katika nafasi ya kuidhinisha makubaliano ya mwisho na tutajitoa. Lakini kwa wakati huu tunahitaji kufanya mambo mwengine, kama kutafuta masoko mapya.
Tatizp ni kwamba Namibia , Lesotho, Botswana na Afrika kusini zina umoja wao wa forodha, yaani Southern Afrikan Customs Union SACU, ulioanzishwa mwaka 1910. Lesotho, Botswana na Swaziland zimetia saini mkataba wa EPA unaojumuisha mataifa ya SADC ambao una vifungu ambavyo Namibia haifurahishwi navyo.
Moja kati ya vifungu hivi vinazuwia mahitaji ya matumizi ya mali ghafi ya ndani katika sekta ya viwanda.Ili kuweza kusaidia viwanda vya ndani, Namibia haitaki kufuta sheria yoyote ambayo inamhitaji mwekezaji kutumia mali ghafi inayotengenezwa nchini humo. Kifungu kingine kinahusika na kuondoa kodi ya mauzo ya nje. Namibia hata hivyo , inataka uhuru wa kutumia kodi ya mauzo ya nje ili kushawishi kutouzwa mali ghafi zake nje ya nchi na kuvipa nguvu viwanda vya ndani kuongeza thamani ya bidhaa zake kabla ya kuziuza nje.
Umoja wa Ulaya umezitaka nchi za SADC kuipatia nafasi sawa wa soko lake , kama nchi hizo za SADC zinavyotoa kwa washirika wengine muhimu wa kibiashara. Mataifa ya SADC kwa sasa yanajadiliana kuhusu makubaliano ya soko huru na India na eneo la MERCOSUR ambalo linajumuisha mataifa ya Brazil , Paraguay , Argentina na Uruguay.