Umoja wa Mataifa wataka uhakika wa usalama Aleppo
18 Oktoba 2016Umoja wa mataifa umesema leo kwamba mpango wa Urusi wa kusitisha mapigano hautakuwa na maana kwamba misaada ya kiutu itaingia katika eneo la mashariki la mji wa Aleppo lililozingirwa kwa sababu Urusi, Syria na makundi mengine yanayopigana hayajatoa uhakika wa usalama kwa wafanyakazi wa kutoa misaada.
Wakati huo huo waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani Thomas de Maiziere amesema juhudi za kupambana na kundi la Dola la Kiislamu nchini Iraq na Syria hazitaongeza kitisho cha mashambulizi nchini Ujerumani.
Akizungumzia hali hiyo, msemaji wa Umoja wa Mataifa Jens Laerke ameitaka Serikali ya Syria pia kubadilisha uamuzi wake wa wiki iliyopita wa kukataa kuruhusu misaada kuingia katika eneo la mashariki la mji wa Aleppo, ambako umoja huo unakadiria kwamba raia 275,000 na waasi wapatao 8,000 wamekwama.
"Tunahitaji kupatiwa uhakika kutoka pande zote katika mzozo huo, sio tu tangazo la upande mmoja , kwamba hili litatendeka . Tunahitaji kila mtu kutoa uhakikisho huo kabla ya sisi kuweza kufanya kitu chochote cha maana kwa upande wa kiut."
Kamati ya kimataifa ya msalaba mwekundu imesema bado haijawa wazi ni muda gani utahitajika kupata uhakikisho huo wa usalama kutoka pande zote, ikiwa ni pamoja na wapiganaji waasi.
Uharibifu wa hospitali
Urusi imesema jana kwamba majeshi ya nchi hiyo na Syria yanasitisha mapigano katika mji wa Aleppo kwa masaa nane siku ya Alhamis kuruhusu raia na waasi kuondoka kutoka katika mji huo, na leo wamesitisha mashambulizi yote ya anga , siku mbili kabla ya muda uliotangazwa.
Laerke aliuambia mkutano wa kila siku wa waandishi habari mjini Geneva kwamba Urusi imeuambia Umoja wa Mataifa kwamba usitishaji mapigano ni kwa masaa nane katika zaidi ya siku moja kamili.
Mashambulizi ya Urusi na Syria yameharibu mahospitali mengi katika mji huo uliozingirwa, ambako watu 406 waliuwawa na 1,384 wamejeruhiwa kati ya Septemba 23 na Oktoba 8, kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa kutokana na ripoti kutoka mahospitali mbali mbali.
Robert Mardini mkurugenzi wa kanda wa kamati ya kimataifa ya msalaba mwekundu ICRC kwa ajili ya mashariki ya mbali na kati , amesema , "makadirio yetu hivi leo ni kwamba kuna makundi karibu 50 ndani ya mashariki mwa Aleppo, na sio tu kuhusu Urusi na serikali ya Syria," ameliambia shirika la habari la Reuters.
Vikwazo vya kiuchumi
Pamoja na hayo kansela wa Ujerumani Angela Merkel amesema haondoi uwezekano wa Urusi kuwekewa tena vikwazo vya kibiashara kutokana na hatua zake nchini Syria.
Mke wa rais wa Syria Asma al-Assad wakati huo huo amesema amekataa maombi kadhaa ya kukimbia vita pamoja na watoto wake , kwa mujibu wa mahojiano aliyofanya na kituo cha televisheni cha Russia 24 yaliyorushwa hewani leo Jumanne.
Nae waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani Thomas de Maiziere amesema maafisa wanatarajia wapiganaji wa IS kutoka Ulaya watajaribu kurejea nyumbani wakati kundi hilo likikabiliwa na kupoteza maeneo , lakini maafisa wanaifanyia kazi hali hiyo kupunguza kitisho cha usalama.
Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre / ape / afpe
Mhariri: Daniel Gakuba