UN: Hatua ya kwanza yafikiwa juu ya usafirishaji wa nafaka.
14 Julai 2022Guterres ameeleza kwamba hatua hiyo imefikiwa kwenye mazungumzo ya mjini Istanbul kati ya wajumbe wa Urusi na Ukraine. Wajumbe wa Umoja wa Mataifa na Uturuki pia walishiriki kwenye mazungumzo hayo.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameelezea matumaini ya kupatikana makubaliano rasmi wiki ijayo. Amesema kwa jumla pana makubaliano juu ya mpango wa Umoja wa Mataifa wa kusafirisha mamilioni ya tani za nafaka kutoka Ukraine na kufikisha kwenye masoko ya kimataifa na pia kuiwezesha Urusi kuuza nje nafaka na mbolea. Vikwazo vya kimataifa dhidi ya Urusi vimeongeza bei ya mbolea, ambayo inasababisha kupanda kwa bei ya chakula.
Naye waziri wa ulinzi wa Uturuki Hulusi Akar aliyeshiriki kwenye mazungumzo hayo amefahamisha kuwa pande zote zimekubaliana juu ya udhibiti wa pamoja kwenye bandari na kwenye njia nyingine ili kuhakikisha usafirishaji salama. Mpango huo uliopendekezwa na Umoja wa Mataifa utawezesha kusafirishwa shehena hizo za nafaka kupitia njia maalum, zitakazoepuka maeneo ya hatari.
Ukraine yahangaika kusafirisha ngano yake
Takriban tani milioni 22 za nafaka zimezuiliwa nchini Ukraine, na shinikizo lilikuwa likiongezeka kila uchao la kutafuta suluhu ambayo ingewezesha tena kusafirisha ngano kutoka kwenye maghala ya Ukraine kwa wakati kwa ajili ya kuweka nafasi ya kuhifadhi nafaka zitakazopatikana katika mavuno yajayo.
Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo FAO, limesema vita vya nchini Ukraine vinahatarisha juhudi za usambazaji wa chakula kuelekea kwenye mataifa mengi yanayoendelea, na hivyo kusababisha kuongezeka kwa bei ya chakula duniani kote na hali hiyo inaweza kuzidisha baa la njaa kwa hadi watu milioni 181.
Chanzo: https://p.dw.com/p/4E5ag