Umoja wa Mataifa wasema haki za binaadamu zimedorora Urusi
18 Septemba 2023Hali jumla ya haki za binaadamu imekuwa mbaya nchini Urusi tangu Moscow ilipoivamia Ukraine mwaka jana. Hayo ameyasema Jumatatu Mariana Katzarova, mtaalamu wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa, huku akilaani vitendo vya mateso vya mara kwa mara ikiwa ni pamoja na unyanyasaji wa kijinsia.
Katzarova amebainisha kwamba Urusi imekuwa ikishuhudia hali mbaya zaidi ya haki za binaadamu katika miongo miwili iliyopita, kwa kiwango fulani ikiwa ni urithi wa vita vya Chechnya vilivyomalizika mwaka 2009.
Mtaalamu huyo amesema Urusi inauhujumu uhuru wa mahakama.
Katzarova, ambaye mwezi Aprili aliteuliwa na Baraza la Haki za Binaadamu la Umoja wa Mataifa, kuwa mfuatiliaji wa kwanza kabisa wa hali ya haki nchini Urusi, ameeleza kuwa mamlaka za Urusi zimeminya vikali uhuru wa kukusanyika kwa amani na kujieleza, iwe mtandaoni au nje ya mtandao.