Umoja wa Mataifa walaani mashambulizi ya waasi Syria
31 Oktoba 2016Staffan de Mistura amesema ameshtushwa na idadi kubwa ya makombora yanayorushwa katika maeneo ya raia katika vitongoji vilivyo chini ya udhibiti wa serikali mjini Aleppo. Mjumbe huyo maalumu wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Syria amesema kwamba "wale ambao wanasema kwamba hili lilimaanisha kupunguza mzingiro mashariki mwa Aleppo, wanapaswa kukumbuka kwamba hakuna jambo linalohalalisha matumizi ya silaha zenye kudhuru watu, zikiwemo silaha nzito kwa maeneo ya raia huu unaweza kuchukuliwa ni uhalifu wa kivita" .
Waasi nchini Syria jana jumapili waliendelea na urushaji wa makombora yaliyowaua watu saba wakiwemo watoto watatu, na kusafisha njia wakiwa na magari ya mabomu na mizinga na kuingia katika eneo jipya mashariki mwa mji huo. Serikali ya Syria imedai kwamba wapiganaji wa upinzani wametumia gesi ya sumu.
Idadi ya vifo katika siku tatu za mashambulizi makali imefikia watu 41 wakiwemo watoto 16, kwa mujibu wa shirika la uangalizi wa haki za binadamu la nchini humo.
Makombora hayo ya jana jumapili (30.10.2016 ) yanakuja ikiwa ni siku ya tatu ya mashambulizi ya wapiganaji ambayo yanalenga kuvunja mzingiro wa serikali katika maeneo ya waasi mashariki mwa wilaya za Aleppo, zaidi yakilenga kuviondoa vikosi vya serikali katika uwanja wa mapambano.
Eneo la mashariki mwa Aleppo limekuwa katika mzingiro tangu mwezi Julai na kuwakwamisha raia karibu 275,000. Urusi na serikali ya Syria wamesimamisha mashambulizi yao ya anga katika eneo hilo tangu wiki iliyopita ili kuruhusu zoezi la kuwaokoa wagonjwa na raia waliojeruhiwa. Lakini zoezi hilo halikuwezekana na jitihada za usambazaji wa vifaa vya tiba na chakula katika maeneo yaliyo katika mzingiro nazo zimesimamishwa. Hadi sasa vikosi vya serikali vimeendelea na mashambulizi ya ardhini dhidi ya maeneo ya waasi.
De Mistura amesema raia wa pande zote mbili za Aleppo wameteseka vya kutosha na mashambulizi yasiyokuwa na maana zaidi ya kuharibu mji huo, akiongeza kwamba "sasa wanahitaji usitishaji mapigano wa mji huo wa kale wa Syria".
Katika mkanda wa video uliorushwa na kundi lenye mafungamano na al-Qaeda la Fatah al-Sham zimeonyesha wapiganaji hao wakisonga mbele katika vitongoji vya karibu katika mizinga na magari mengine ya kijeshi. Kiongozi wa kundi hilo Abu Mohammed al-Golani ameonekana katika mkanda huo akijadiliana na kamanda wa kikosi juu ya mapambano. Wapiganaji hao walitegemea zaidi magari ya mabomu ili kuvunja ulinzi wa adui zao yani vikosi vya serikali.
Mkuu wa Shirika la Kuchunguza Haki za Binadamu nchini Syria lililo na makao yake nchini Uingereza Rami Abdurahman amesema kiasi ya askari 1000 wa vikosi vya jeshi la serikali wamewasili mjini Aleppo kutoka katikati mwa Syria siku ya jumamosi ili kuongeza nguvu katika mapambano huku akikadiria idadi ya wapiganaji kufikia 2500. Ameongeza kwamba raia kadhaa wamepata shida ya kupumua kutokana na mashambulizi ya jumapili ingawa hakuthbitisha kama kulikuwa na matumizi ya gesi ya sumu.
Mwandishi: Sylvia Mwehozi/AP
Mhariri: Daniel Gakuba