1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Mataifa waitaka Mali kufanya uchaguzi Februari

25 Oktoba 2021

Ujumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambao uliizuru Mali kutathmini hali ya usalama nchini humo, umetoa wito kwa viongozi wa serikali ya mpito kupanga tarehe ya uchaguzi utakaofanyika mwezi Februari.

https://p.dw.com/p/42992
Mali - Delegation des UN-Sicherheitsrats in Bamako
Picha: Présidence de la République du Mali

Wito huo umetolewa ili kutekeleza makubaliano yaliyofikiwa na viongozi wa Jumuiya ya Uchumi ya nchi za Afrika Magharibi, ECOWAS baada ya mapinduzi ya mwaka uliopita.

Ujumbe huo ulioongozwa na Balozi wa Kenya kwenye Umoja wa Mataifa, Martin Kimani, mwishoni mwa juma ulikutana na wadau muhimu katika makubaliano hayo, yakiwemo mashirika ya vyama vya kiraia, vyama vya kisiasa, makundi ambayo yamesaini makubaliano ya amani, waziri mkuu wa Mali pamoja na Rais wa serikali ya mpito, Kanali Assimi Goita.

Matakwa ya mageuzi ya kisiasa na kikatiba

Akizungumza na waandishi habari hapo jana mjini Bamako, Balozi Kimani amesema wameguswa na matakwa ya wananchi wa Mali kuhusu mageuzi ya kisiasa na kikatiba na kwa sasa wanasubiri kumalizika kwa kipindi cha mpito ambacho kinapaswa kuielekeza nchi hiyo katika uchaguzi.

''Tunataka kuielewa hali iliyopo Mali, ili tuweze kuujulisha mkutano wetu utakaofanyika New York. Kama nchi ya Afrika mwenzetu, hali ya Mali na Ukanda wa Sahel ni muhimu sana kwa Kenya. Tuna wasiwasi na hali ya kukosekana kwa usalama inayoendelea kwenye nchi yenu, na kuongezeka kwa vitendo vya kigaidi na athari zake kwa raia wa Mali,'' alifafanua Kimani.

Mali Oberst Assimi Goita, neuer Übergangspräsident
Rais wa mpito wa Mali, Assimi GoitaPicha: Xinhua/imago images

Hata hivyo baada ya mkutano wao na ujumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, viongozi wa mpito wa Mali wamesema watathibitisha tarehe ya uchaguzi baada ya kufanyika mazungumzo ya mwezi Desemba miongoni mwa makundi ya Mali yanayohusika ili kuamua njia ya kuelekea kwenye demokrasia.

Balozi wa Niger katika Umoja wa Mataifa, Abdou Abarry ambaye alikuwa sehemu ya ujumbe huo, amesema viongozi wa Mali wamewaeleza kuhusu umuhimu wa mikutano hiyo kama sharti la kufanyika uchaguzi. Abarry amesema hawapingi kufanyika kwa mikutano hiyo, lakini wanasisitiza isicheleweshe kumalizika kwa kipindi cha mpito na kuwapa wananchi wa Mali fursa ya kuwachagua viongozi wao.

Viongozi wa mpito wataondoka madarakani 

Balozi huyo wa Niger amesema Kanali Goita ameuhakikishia ujumbe huo kwamba viongozi wa mpito hawatobakia madarakani kwa muda mrefu na ahadi zozote zinazotolewa na viongozi hao zitakuwa kwa maslahi ya wananchi wa Mali.

Mabalozi wa Umoja wa Mataifa pia wameelezea wasiwasi wao kuhusu hali ya usalama nchini Mali. Balozi wa Ufaransa kwenye Umoja wa Mataifa, Nicolas de Riviere amesema viongozi wa Mali wamesisitiza kwamba wanaongeza mkazo katika changamoto za kiusalama na kwamba kikosi cha Umoja wa Mataifa cha kulinda amani nchini Mali, MINUSMA kiko tayari kusaidia, hasa kwenye eneo la katikati ya Mali ambako kuna kitisho kikubwa cha ugaidi.

Kanali Goita alichukua madaraka Agosti, 2020 baada ya kumpindua kiongozi aliyechaguliwa kidemokrasia, Ibrahim Boubacar Keita. Baada ya kuapishwa kuwa rais wa mpito wa Mali mwezi Juni, Goita aliahidi kuirudisha nchi hiyo kwenye utawala wa kiraia kwa kuandaa uchaguzi utakaofanyika mwezi Februari mwaka ujao wa 2022.

(AP, Reuters)