1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Mataifa wafichua njama za kijeshi nchini Libya

Admin.WagnerD25 Mei 2020

Umoja wa Mataifa umefichua mpango wa siri unaohusisha wapiganaji binafsi ikiwemo kutoka mataifa ya magharibi walioingia nchini Libya kumsaidia kamanda wa vikosi vya jeshi la mashariki ya nchi hiyo Khalifa Haftar

https://p.dw.com/p/3cj2u
Libyen Tripoli | Portrait | GNA Kämpfer
Picha: picture-alliance/dpa/A. Salahuddien

Kulingana na ripoti ya wataalamu wa Umoja wa Mataifa iliyoonwa na shirika la Habari la DPA, zaidi ya watu 20 wenye ujuzi wa kijeshi kutoka mataifa ya Australia, Ufaransa, Malta, Afrika Kusini, Uingereza na Marekani wanahusika na mpango huo wa siri wa kumuunga mkono Jenerali Khalifa Haftar.

Libyen Freischärler mit Waffen
Picha: picture-alliance/dpa/M. Gambarini

Ripoti hiyo imesema watu hao ambao ni wafanyakazi wa kampuni binafsi za kijeshi waliingia Libya mwishoni mwa mwezi Juni mwaka 2019 kwa kutumia ndege ya mizigo kutokea Jordan kwa madai ya kuhusika na shughuli za utafiti wa kisayansi nchini humo.

Umoja wa Mataifa umesema taarifa hizo zilikuwa za uongo na kundi hilo la watu lilipelekwa Libya kuusaidia upande wa Haftar kwa kuzuia meli za Uturuki ambao husafirisha msaada wa kijeshi kwenda serikali ya mjini Tripoli pamoja kudhbiti usambazaji wa silaha kwa upande huo hasimu.

Wataalamu wa Umoja wa Mataifa wamefichua kuwa mpango huo uliratibiwa na kampuni zenye makao yake huko Muungano wa Falme za Kiarabu na ulihusisha pia ununuzi wa helikopta za kijeshi zilizopelekwa mjini Benghazi, mji unaodhibitiwa na Haftar.

Taarifa kuhusu uwepo wa mpango kama huo ni ufichuzi wa hivi karibuni kabisa wa kuhusika kwa madola ya kigeni katika vita nchini Libya.

Umoja wa Mataifa umerikodi mara kadhaa uwepo wa mamluki wa kigeni wanaofanya kazi nchini Libya pamoja na kuendelea kwa ukiukwaji mkubwa wa marufuku ya kuingiza silaha nchini Libya ikiwemo kutoka Uturuki, taifa linaloiunga mkono serikali ya mjini Tripoli.

Mamluki wa Urusi wakimbia mapigano 

Libyen Regierungssoldaten
Picha: picture-alliance/AA/H. Turkia

Katika hatua nyingine wapiganaji wa Urusi wanaomuunga mkono Jenerali Haftar wamelazimika kuondoka kutoka mji mmoja wa kusini ya Libya baada ya kusalimu amri katika mapambano ya makali yanayoendelea ya kuwania udhibiti wa mji mkuu, Tripoli.

Meya wa mji wa Bani Walid, Salem Alaywan amesema wapiganaji wa Urusi pamoja na vifaa vyao vya kijeshi wamepelekwa kwenye mji huo kutoka katikati ya Tripoli.

Upande wa Haftar umepinga madai hayo ukisema hakuna wapiganaji wa kigeni wanaoshiriki vita vinavyoendelea nchini Libya.

Taarifa za kuondolewa wanajeshi wa kirusi ni pigo jingine kwa Jenerali Haftar na washirika wake wa kigeni ambao kwa miezi 13 wanaendesha kampeni ya kijeshi ya kuukamata mji wa Tripoli.

Katika siku za karibuni Haftar na washirika wake wakiongozwa na Urusi, Misri na Muungano wa Falme za Kiarabu  wamepoteza maeneo muhimu baada ya kuzidiwa nguvu na serikali ya mjini Tripoli inayoungwa mkono kwa sehemu kubwa na Uturuki.

Mwandishi: Rashid Chilumba

Mhariri: Idd Ssesanga