Umoja wa Mataifa wathibitisha kubakia nchini Afghanistan.
6 Mei 2023Umoja wa Mataifa umethibitisha tena ahadi yake ya kubakia nchini Afghanistan. Haya ni kulingana na mapitio ya tathmini ya operesheni zake nchini humo, katika wakati ambapo Taliban imewazuia wanawake kufanya kazi kwenye mashirika ya umoja huo. Umoja huo ulizindua tathmini iliyoangazia ikiwa itaendelea kufanya kazi na Taliban na hasa baada ya zuio hilo na hatimaye jana kutoa tamko hilo. Msemaji wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa amewaambia waandishi wa habari kwamba ujumbe wa umoja huo nchini Afghanistan, UNAMA, utabakia nchini Afghanistan, kwa ajili ya raia wote wa nchi hiyo. Katika taarifa yake, shirikal la UNAMA limelaani hatua ya kuwazuia wanawake kufanya kazi. Limesema inadhoofisha majukumu ya shirika hilo la Umoja wa mataifa pamoja na uwezo wa kuwafikia watu wote. UNAMA imeahidi kuendelea kujadiliana na serikali ya Taliban namna watakavyoshirikiana.