Umoja wa Mataifa kuipigia kura Syria
9 Desemba 2016Canada ndiyo iliyoandaa rasimu hiyo, kama sehemu ya juhudi za kumaliza mvutano uliopo kuhusu Syria, miongoni mwa wanachama 193 wa baraza kuu la umoja huo.
Urusi na China wiki hii zilipinga kwa kutumia kura ya turufu, azimio la kutaka kusitishwa kwa mapigano mjini Aleppo kwa siku saba, mji ambao unakaribia kukombolewa na vikosi vya serikali.
Hii ni mara ya sita kwa Urusi, mshirika wa karibu wa Rais wa Syria, Bashaar al-Asaad, kutumia kura hiyo kupinga mapendekezo ya baraza hilo, yanayoihusu Syria.
Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa linategemewa kulipigia kura azimio hilo ambalo linadai kile ilichokitaja kama "kusitishwa kikamilifu kwa mashambulizi yoyote dhidi ya raia", pamoja na kufunguliwa maeneo yaliyozingirwa.
Naye mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Syria, Staffan de Mistura, akizungumza na wajumbe wa baraza hilo katika mkutano mfupi wa faragha amesema hisia ya umoja imedhihirika katika mkutano huo.
"Sidhani kama nitakuwa ninatafsiri kupindukia, lakini kuna hisia ya umoja iliyojitokeza katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa leo, pengine inatokana na kile alichokieleza balozi wa Uhispania, kwamba ingawa kuna wakati huwa tunatafautia lakini pia kuna wakati ambapo tunalazimika kuwa wamoja, pale tunapotafakari kuhusu nani hasa anayeathirika na mgogoro huu," amesema Staffan de Mistura.
Lakini balozi wa Uingereza kwa Umoja wa Mataifa, Matthew Rycroft , amesema Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limechelewa mno kuchukuwa hatua madhubuti nchini Syria.
De Mistura, amezungumzia pia juu ya mkutano wake ujao na Rais mteule wa Marekani Donald Trump, baada ya kushiriki katika mkutano huo wa Baraza Kuu la Umoja wa Maatifa kuhusu Syria.
De Mistura amesema wakati umefika wa kurudi tena katika meza ya mazungumzo ya kisiasa yanayoihusu Syria, kufuatia tangazo la Urusi kwamba vikosi vya serikali ya Syria vimesitisha operesheni zote za kivita mashariki mwa Aleppo.
Mjumbe huyo ameyasema hayo kufuatia kauli ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergei Lavrov, ya kwamba jeshi la Syria, ambalo limefanikiwa kukomboa maeneo makubwa ikiwa ni pamoja na mji mkongwe wa Aleppo siku za karibuni, limesitisha mashambulizi ili kuwapa fursa raia kuyakimbia maeneo yanayodhibitiwa na waasi. Lavrov pia amesema Urusi imewasaidia zaidi ya watu 8,000 kutoka eneo la mashariki mwa Aleppo lililokuwa chini ya waasi.
Lakini, maripota wa shirika la habari la Reuters waliopo katika eneo linalodhibitiwa na serikali wamesema milio ya mabomu bado ilikuwa ikisikika wakati wa kauli hiyo ya waziri wa Urusi.
Katika siku 26 zilizopita, zaidi ya watu 800 wameuawa na wengine 3,500 wamejeruhiwa mashariki mwa mji wa Aleppo, kutokana na mashambulizi yanayofanywa na vikosi vya serikali.
Mwandishi: Yusra Buwayhid/rtre/afpe
Mhariri: Daniel Gakuba