Umoja wa Mataifa kupiga kura kuiwekea vikwazo Syria
28 Februari 2017Rasimu ya azimio hilo iliyoandaliwa na Marekani, Uingereza na Ufaransa inakusudia kuwawekea vikwazo raia 11 wa Syria pamoja na taasisi 10 zinazohusishwa na mashambulizi hayo yaliyofanyika kwa kutumia silaha za sumu katika mgogoro uliochukua karibu miaka sita sasa.
Hatua hiyo pia inalenga kuzuia mauzo ya vifaa vya kijeshi pamoja na ndege za kivita kwa jeshi la Syria au serikali ya nchi hiyo.
Pendekezo hilo linafuatia uchunguzi uliofanywa na Umoja wa Mataifa uliomalizika Oktoba mwaka jana ulioihusisha Syria na matumzi ya mabomu ya mapipa kwa kutumia ndege zake za kivita kuyalenga maeneo matatu yaliyokuwa yakishikiliwa na makundi ya upinzani katika kipindi cha mwaka 2014 na 2015.
Uchunguzi huo uliofanywa na Umoja wa Mataifa ukishirikisha shirika linalohusika na kuzuia matumizi ya silaha za sumu (OPCW) pia ulibaini kundi la itikadi kali linalojiita Dola la Kiisilamu lilitumia silaha za sumu katika mashambulizi yake mnamo mwaka 2015.
Balozi mdogo wa Urusi katika Umoja wa Mataifa, Vladimir Safronkov alisema ijumaa iliyopita kuwa Urusi itatumia kura yake ya turufu kupinga hatua hiyo kwa sababu imeegemea upande mmoja na hakuna ushahidi wa kutosha.
Syria yakanusha matumizi ya silaha za sumu
Serikali ya Syria imekuwa ikiendelea kukanusha matumizi ya silaha za sumu katika vita nchini humo ambayo tayari imewaua watu 310,000 tangu ilipoibuka Machi 2011.
Wakati huohuo mashambulizi ya anga yaliyofanywa katika jimbo la Idlib hapo jana yamewaua kiasi ya watu 11 na kutia doa mazungumzo ya amani ya Syria yaliyosimamiwa na Umoja wa Mataifa yaliyofanyika Geneva yakishirikisha upande wa serikali na makundi ya waasi.
Kuna taarifa ambazo hazijathibitishwa zinazodai kuuawa afisa wa juu wa kundi la itikadi kali la al-Qaeda katika mashambulizi ya anga yaliyofanywa katika jimbo la Idlib.
Kundi la Ujasusi la SITE linalofuatilia makundi ya itikadi kali limesema Abdullah Muhammad Rajab Abdulrahman ambaye ni kiongozi msaidizi wa kiongozi wa al-Qaeda Ayman al-Zawahiri anaweza kuwa ameuawa katika mashambulizi hayo yaliyofanywa na ndege za kivita za Marekani.
Jimbo la kaskazini mashariki linadhibitiwa zaidi na kundi la al-Qaida lenye mafungamano na kundi la waasi ambako mamia ya raia wa Syria waliolazimika kuhama maeneo yao ya makazi wanaishi kama wakimbizi katika eneo hilo.
Mwandishi: Isaac Gamba/AFPE/APE
Mhariri : Iddi Ssessanga