Umoja wa Mataifa watahadharisha juu ya ongezeko la joto
18 Mei 2023Matangazo
Shirika hilo limesema joto litaongezeka kwa kiwango kikubwa kutokana na mchanganyiko wa athari za joto la baharini na hewa zinazochafua mazingira.
Kwa mujibu wa shirika hilo, dunia inapaswa kujitayarisha kwa sababu kuna uwezekano wa asilimia 98 wa joto kuwa kali mno.
Katibu Mkuu wa shirika hilo la utabiri wa hali ya hewa la Umoja wa Mataifa, Petteri Taalas, amesema mfumo wa joto wa El Nino unatarajiwa kujijenga katika miezi ijayo na hali hiyo itachanganyika na athari za mabadiliko ya tabia nchi zinazosababishwa na binadamu na kuielekeza dunia katika mkondo usiotabirika.
Taalas, ametahadharisha kwamba dunia itafikia kiwango cha nyuzijoto 1.5 mara kwa mara na hali hiyo itaathiri afya, upatikanaji wa chakula,uhifadhi wa maji na mazingira.