Umeme wakatika Tanzania wakati Kimbunga Hidaya kikikaribia
4 Mei 2024Mvua kubwa na upepo mkali vimeripotiwa katika ukanda wa pwani, maeneo ya Mtwara na Lindi, huku utabiri ukisema kuwa jiji la kibiashara la Dar es Salaam, linaweza pia kuathirika. Aidha, mamlaka imewaonya watu kuchukua tahadhari kama kasi ya kimbunga itaongezeka.
Katika nchi jirani ya Kenya, mamlaka ya hali ya hewa imewataka wakaazi wa pwani ya nchi hiyo kuwa katika hali ya tahadhari, wakati eneo hilo likitarajiwa pia kupigwa na Kimbunga Hidaya.
Kaunti zilizotajwa kuwa na hatari ya kuathiriwa na mafuriko kutokana na utabiri wa hali ya hewa pwani ya Kenya ni pamoja na Kilifi, Taita Taveta, Tana River, Kwale na Lamu. Kaunti hizo za Pwani bado hazijaathirika na mvua kubwa inayoendelea kunyesha sehemu nyengine za nchi hiyo, lakini serikali ina wasiwasi wa kutokea mafuriko.