1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umeme wa Jua, nishati mbadala Barani Afrika

16 Agosti 2016

Upatikanaji nishati ni changamoto barani Afrika licha ya kuwepo vyanzo vya nishati mbadala. Nchini Uganda, wananchi wamegundua suluhisho lao wenyewe la kujizalishia nishati kwa msaada wa wafadhili wa kimataifa.

https://p.dw.com/p/1JjDk
Wafanyakazi wakiweka vifaa katika eneo linalojengwa mtambo wa umeme wa jua Nchini IndiaPicha: C.Khanna/AFP/Getty Images

Katika mji wa Soroti ambao una uhaba wa umeme nchini Uganda, wanaume huendesha baiskeli umbali wa kilomita kadhaa kwenda eneo la jirani ili tu waweze kuchaji simu zao. Hii inatakiwa kubadilika kufuatia kujengwa kwa moja kati ya mitambo mikubwa kabisa ya kusambaza umeme wa jua katika nchi za kusini mwa jangwa la Sahara ambako theluthi mbili ya wananchi wake wanaishi bila umeme.

Watu wanaoishi eneo hili la nchi, ambayo ina watu milion 36, wanachanganyikiwa kutokana na kasi ndogo ya ya usambazaji umeme maeneo ya vijijini. Hivyo wanaamua kujiwekea vifaa vitakavyowawezesha kupata umeme wa jua ili wapate mwanga katika nyumba zao na katika biashara zao pia, japo mashine za umeme wa jua hugharimu kiasi cha dola 100 za Kimarekani, hii ikiwa ni changamoto kwani kiwango cha pato la taifa kwa nchi hiyo ni dola 703 kwa mwaka kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa.

Mtambo huu utakapozinduliwa baadaye mwaka huu, utakuwa na uwezo kuzalisha megawati 10 ambazo zitaongezwa katika gridi ya taifa. Inakadiriwa kuzifikia kaya 40,000 na baadhi ya maeneo ya biashara zao katika eneo ambalo nchi yake bado inategemea umeme unaozalishwa kwa kutumia maji, anasema Philip Karumuna, mkandarasi wa mradi huo.

"Kuna jua la kutosha, lakini hatulitumii ipasavyo. Kwa vyovyote vile, serikali inabidi ifanye zaidi," anasema Ambrose Kamukama, fundi mkuu katika mradi huo.

Fundi huyo anaongeza kuwa katika wilaya hiyo ya Soroti, jua huwaka karibu kila siku na hii ndio sababu iliyopelekea kuchaguliwa eneo hili, kwani imezungukwa na majani ambapo ng'ombe huchungwa na punda hucheza. Wilaya hii ipo karibu kilomita 300 kutoka mji mkuu nchi hiyo, Kampala, hivyo hoteli na biashara nyingine ndogndogo hutegemea upatikanaji wa umeme wa uhakika.

Umeme unapokatika, anasema mkazi wa emeo hilo Stephen Okut, inawalazimu waketi na kusubiri kwa masaa kadhaa, hali ambayo inakuwa ngumu kufanya kazi zao kwa wakati.

"Tunaamini umeme huu wa jua utasaidia kutatua tatizo la kukatika kwa umeme," anasema David Mugoda, meneja wa Hoteli ya Soroti, ambayo hulazimika kuwasha jenereta la gesi mara kwa mara pale umeme unapokatika, jambo ambalo humaliza kabisa faida yake, kwani bidhaa kama maziwa yanayokuwa katika friza yanaharibika

"Umeme unakatika mara kwa mara na unapokatika unaweza ukalaani maisha yako kwa sabau unapokuwa unahitaji sana, ndipo nao hukatika." Anasema mfanyabiashara huyo.

Bildergalerie Solarenergie - Elfenbeinküste
Wakazi wa kijiji kisicho na umeme sehemu ya huduma ya kupiga simuPicha: AFP/Getty Images/S. Kambou

Mradi huu unadhaminiwa na GET FiT chini ya Umoja wa Ulaya kwa kushirikiana na Ujerumani, Norway na Uingereza. Wakati wa uzinduzi wa mradi huo mwezi Machi, kiongozi wa ujumbe wa Umoja wa Ulaya, Kristian Schmidt, anasema wanatazamia mradi huu "kuwa ni mwanzo tu wa vitu vingi vitakayofuata".

Wataalam wazikosoa Serikali za Afrika

Wataalamu wa masuala ya nishati wanasema miradi kama hii inaweza kusaidia kuboresha upatikanaji wa nishati hii katika nchi za Afrika. Mwaka 2014, nchini Rwanda, nje kidogo ya mji mkuu Kigali kulifanywa mradi kama huu ambao ulichangia megawati 8.5 za umeme katika gridi ya taifa na ambao ulishaidia upatikanaji wa umeme kwa karibu asilimia 6.

Lakini mradi huu wa Uganda ni wa kwanza kwa ukubwa katika nchi za kusini mwa jangwa la Sahara ukiacha ule wa Afrika ya Kusini.

"Kama kukiwa na mipango mizuri, serikali za Afrika zinaweza kuongeza uzalishaji wa nishati," anasema Dickes Kamugisha ambaye ni kiongozi wa taasisi iitwayo Africa Insitute for Energy Governance.

"Hatutakiwi kuisifia serikali kwa kujenga mabwawa" alisema akirejea hatua ya serikali ya Uganda ambayo imekuwa ikitumia pesa nyingi kujenga mabwawa ya kuzalisha umeme. Na kwa mujibu wa Kamugisha, ufumbuzi kwa watu masikilini lazima iwe ni umeme wa gesi."

Mwandishi: Celina Mwakabwale/AP

Mhariri: Mohammed Khelef