Ulaya yasitasita kuiongezea vikwazo Urusi
17 Oktoba 2016
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari wakati wa mkutano wa mawaziri hao mjini Luxembourg Jumatatu, Mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya Federica Mogherini amesema hakuna nchi mwanachama iliyopendekeza kuiongezea Urusi vikwazo zaidi ya vile ilivyowekewa kutokana na mchango wake katika mgogoro wa Mashariki mwa Ukraine. Hali hiyo inakwenda kinyume na wito uliokuwa umetolewa jana na mawaziri wa mambo ya nje wa Marekani na Uingereza baada ya mazungumzo mjini London.
Bi Mogherini amesema kinachowezekana ni vikwazo zaidi dhidi ya serikali ya Rais Bashar al-Assad wa Syria, akiongeza kuwa tayari mjadala unaendelea kuhusu hatua hizo.
Ulaya katika nafasi nzuri ya ushauri
Federica Mogherini amesema anaona fahari kuwa Umoja wa Ulaya hauhusiki kijeshi katika vita vya Syria, hali ambayo amesisitiza inauweka umoja huo katika nafasi ya kuweza kuwahimiza wadau wa vita hivyo kusitisha uhasama, kutafuta suluhisho la kudumu na kuwezesha upelekwaji wa msaada wa kiutu.
Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank Walter Steinmeir amesema vikwazo zaidi dhidi ya Urusi haviwezi kuwapunguzia matatizo raia wanaoteseka katika mji w Aleppo, akisema hayuko peke yake mwenye mawazo kama hayo. Yeye pia amelielekeza shinikizo upande wa serikali ya Syria.
Msimamo kama huo umekaririwa na waziri wa mambo ya nje wa Luxembourg Jean Asselborn, ambaye amesema kujadiliana juu ya vikwazo vipya dhidi ya Urusi ingekuwa kazi bure, kwani haingekuwa rahisi kuafikiana juu ya suala hilo, na kwa maoni yake huu sio wakati mwafaka kwa mjadala huo.
Uingereza yajitutumua
Boris Johnson, waziri wa mambo ya nje wa Uingereza ambaye hapo jana alikubaliana na mwenzake wa Marekani juu ya ulazima wa kuizidishia vikwazo Urusi, alikuwa na msimamo mkali zaidi, akisema maafa katika mji wa Aleppo ni aibu kwa ubinadamu, na kwamba ilikuwa muhimu kuendelea kumbana rais Assad na washirika wake.
''Tunatafakari njia za kumuongezea shinikizo rais Bashar al-Assad na vibaraka wanaomuunga mkono, nikiwa na maana ya Urusi na Iran bila shaka. Kama anavyojua kila mtu yapo mengi tunayoyafanya, kuanzia vikwanzo vya kiuchumi hadi mbinyo wa kidiplomasia kwa njia moja au nyingine.'' Amesema Johnson.
Mwenzake wa Ufaransa Jean Marc Ayrault alikubaliana na maoni kama hayo.
Mkutano wa wakuu wa nchi za Umoja wa Ulaya utakaofanyika Alhamis wiki hii mjini Brussels unatabiriwa kuwa na kibarua kigumu katika kuutathmini uhusiano baina ya umoja huo na Urusi, huku matumaini yoyote kuwa mambo yangetengamaa haraka baina ya pande hizo yakififia kutokana na mzingiro dhidi ya Aleppo, unaofanywa na serikali ya Syria kwa msaada wa Urusi.
Mwandishi: Daniel Gakuba/afpe, rtre
Mhariri: Mohammed Khelef