Ulaya yaishutumu vikali Marekani katika mkutano wa Munich
16 Februari 2019Akizungumza jana jioni katika mkutano huo wa Munich, Maas aliwaambia wajumbe wa mkutano huo kuwa kuongezeka kwa nguvu za China kunahitaji nchi za Ulaya na Marekani kufanya kazi kwa pamoja, akigusia pia hatua ya Trump ya kuongeza bei ya bidhaa za chuma kama jambo linalotishia nafasi za ajira Ulaya.
Maamuzi ya Marekani yatajwa hayana tija
Waziri huyo ya mambo ya kigeni wa Ujerumani pia ameishutumu Marekani kwa kujiondoa kutoka mkataba wa kinyuklia uliofikiwa kati ya Iran na nchi zenye nguvu zaidi duniani akisema Ujerumani, Ufaransa na Uingereza zinajaribu kuyadumisha makubaliano hayo kwani yakisambaratika, basi kanda ya Mashariki ya Kati huenda ikatumbukia katika mizozo zaidi.
Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Federica Mogherini amesema umoja huo unalenga kuyadumisha makubaliano hayo yanayoidhibiti Iran kutoendelea na mpango wake wa kuunda silaha za kinyuklia akiongeza ni muhimu kwa usalama wa Ulaya.
Awali, makamu wa Rais wa Marekani Mike Pence alikuwa ameishutumu Iran kwa kile alichokitaja inapnaga mauaji mapya ya Halaiki ya Wayahudi kwa kuendelea kuwa hasimu wa Israel na kuingilia mizozo ya Syria, Lebanon, Iraq na Yemen.
Kaimu waziri wa ulinzi wa Marekani Patrick Shanahan kwa upande wake amesema Marekani inataka kuunga mkono vita dhidi ya wanamgambo wenye itikadi kali wa Dola la Kiislamu katika kanda ya Mashariki ya Kati mbali na Iraq na Syria.
Akizungumza katika ufunguzi wa mkutano wa Munich, Shanahan amezitaja Afghanistan, Ufilipino na kanda ya Sahel kama maeneo ambayo wanamgambo wenye itikadi kali wamekita ngome zao na wanahitaji kuangamizwa.
Marekani itaendelea kuwa mshirika katika vita dhidi ya IS
Shanahan ameendelea kusema hata baada ya Marekani kuyaondoa majeshi yake nchini Syria, itaendela kuwaunga mkono washirika wake katika kanda hiyo kufanikisha vita dhidi ya wanamgambo wenye itikadi kali.
Naye waziri wa ulinzi wa Ujerumanii Ursula von der Leyen amesema sura ya kundi la wanamgambo wenye itikadi kali wa Dola la Kiislamu IS inabadilika sasa baada ya kupoteza eneo kubwa la ngome zao nchini Iraq na Syria.
Von der Leyen na mwenzake wa Uingereza Gavin Williamson ndiyo waliozindua rasmi hapo jana mkutano huo wa kiusalama huku viongozi 30 wa nchi na serikali pamoja na mawaziri 90 wakitarajiwa kuhudhuria mkutano huo wa siku tatu.
Miongoni mwa mada zinazotarajiwa kujadiliwa ni pamoja na mahusiano ya kikanda, kuendelea kuongezeka kwa mzozo kati ya Urusi na nchi za magharibi na mizozo inayoendelea Mashariki ya Kati na mchakato wa Uingereza kujiondoa kutoka Umoja wa Ulaya miongoni mwa ajenda nyingine.
Mwaandaji wa mkutano huo, Wolfgang Ischinger amesema bara Ulaya linapaswa kujiandaa vilivyo inapokuja katika sera za kiusalama na za ulinzi akiongeza kuwa kwa muda sasa Ulaya imekuwa ikijihadaa kuwa imezingirwa na marafiki na washirika.
Mwandishi: Caro Robi/ap/dpa/afp
Mhariri: Josephat Charo