Ulaya yaanza kutoa chanjo ya corona
27 Desemba 2020Dozi za kwanza za chanjo ya Pfizer-BioNTech ziliwasili kwenye mataifa ya Umoja wa Ulaya zikiwemo Italia, Uhispania na Ufaransa ambazo zimeathiriwa vibaya na virusi vya corona, tayari kwa ajili ya kusambazwa kwenye majumba ya kuwatunzia wazee na kwa wafanyakazi wa huduma za afya.
Kuthibitishwa kwa chanjo hiyo kumeongeza matumani kwamba mwaka 2021 unaweza kuleta ahuweni dhidi ya janga la COVID-19, ambalo hadi sasa limeshaangamiza maisha ya watu milioni 1.7 tangu liibuke nchini China mwaka jana.
Chanjo kwenye mataifa yote 27 wanachama wa Umoja wa Ulaya zimepangwa kuanza kutolewa leo (Jumapili, 27 Disemba), baada ya mamlaka kuiidhinisha chanjo hiyo ya Pfizer-BioNTech tarehe 21 Disemba.
Lakini mataifa mengine yalianza chanjo hiyo tangu Jumamosi (Disemba 26), ambapo bibi wa miaka 101 anayeishi nyumba ya kutunzia wazee alikuwa mtu wa kwanza nchini Ujerumani kuchomwa chanjo hiyo, huku pia Hungary na Slovakia nazo zikianza kutoa chanjo kwa watu wao.
Mataifa hayo matatu ya Umoja wa Ulaya yaliungana na China, Urusi na Uingereza, Canada, Marekani, Uswisi, Serbia, Singapore na Saudi Arabia, ambazo tayari zilishaanza kampeni za kutowa chanjo.
Waziri wa mambo ya kigeni wa Italia, Luigi Di Maio, aliwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kuchoma chanjo hiyo, akiwaambia kwamba ndiyo njia ya "kurejesha uhuru wetu, tutaweza tena kukumbatiana."
WHO yaonya dhidi ya kuendelea kuzuka majanga ya virusi
Hata hivyo, katika ujumbe wake kwa njia ya video kuelekea siku ya kwanza ya kimataifa ya Utayarifu wa Chanjo, mkuu wa Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO), Tedros Adhanom Ghebreyesus, alisema umefika wakati sasa dunia ijifunze kutokana na yale yaliyojiri kwenye janga la COVID-19.
"Historia inatuambia kwamba hili halitakuwa janga la mwisho, na kwamba majanga kama haya ndio ukweli uhalisia wa maisha," alisema Tedros.
"Jitihada zozote za kuimarisha afya ya mwanaadamu zitashindwa isipokuwa tu ziwe zinazingatia mahusiano tete baina ya wanaadamu na wanyama, na kitisho kilichopo cha mabadiliko ya tabianchi, ambacho kinaifanya sayari yetu ya dunia izidi kuwa na sifa ya kutokuweza viumbe kuishi," aliongeza.
AFP