1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ukuta wa Berlin uliporomoka pia barani Afrika

8 Novemba 2019

Kuporomoka kwa Ukuta wa Berlin miongo mitatu iliyopita kulikuwa pia ni kuporomoka kwa mifumo michanga ya kisiasa katika mataifa ya Afrika yaliyokuwa ndio kwanza yanaanza kujijenga baada ya kupata uhuru.

https://p.dw.com/p/3SXwK
Deutschland, Brandenburger-Tor, Berlin, Mauer, Grenztruppen 1989
Picha: picture-alliance/G.Schaefer

"Kuporomoka kwa Ukuta wa Berlin hakukuwa tu alama ya mwisho kwa Vita Baridi na mwisho wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Ujerumani. Kwa mataifa yote washirika, kuporomoka kwa Ukuta huu kulikuwa na athari kubwa sana, hasa kwa mataifa ya Kiafrika kama vile Msumbiji, Angola na pia Ethiopia," ndivyo anavyosema aliyekuwa waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Mashariki (GRD) kabla ya kuporomoka kwa ukuta wa Berlin, Marcus Meckel.

Kwa kweli GDR ilikuwa imejenga mahusiano maalum na mataifa kadhaa ya Kiafrika, zikiwemo Ethiopia, Angola, Msumbiji, Guinea-Bissau na Tanzania, na hata vyama vya ukombozi kama SWAPO ya Namibia na ANC ya Afrika Kusini. GDR ilizisaidia nchi na vyama hivi vya ukombozi "kujenga Usoshalisti" kupitia programu maalum za mafunzo, misaada na hata silaha.

Baada ya kuporomoka kwa Ukuta wa Berlin, anakumbuka Markus Meckel, yote hayo yalikatika hapo hapo. Lakini je, kweli mahusiano na mataifa ndugu ya kisoshalisti barani Afrika wakati huo yeye akiwa waziri wa nje wa GDR lilikuwa jambo la maana sana kwa Ujerumani Mashariki?:

"Tulikuwa ndio kwanza tumeandaa uchaguzi huru na kulikuwa kumebakia miezi na wiki chache kabla ya kuungana tena kwa Ujerumani. Nikiwa waziri wa nje, nilijaribu kuliendeleza suala la Afrika, lakini kwenye mazingira kama hayo haikuwezekana kuwa rahisi," anasema Meckel.

Kwa mataifa na vyama vya ukombozi barani Afrika hiyo ilimaanisha kwamba Jamhuri ya Kidemokrasia ya Ujerumani alikuwa mshirika aliyepotea. Kuanzia hapo, mataifa hayo yalipaswa kujipanga upya kusaka washirika kwengineko ulimwenguni.

Matokeo mabaya kwa Waafrika

Adelino Massuvira Joao
Adelino Massuvira Joao Picha: DW

Wakati Ukuta wa Berlin unaporomoka na hivyo kuporomoka pia Ujerumani ya Kisoshalisti, upande wa mashariki kulikuwa na takribani wanafunzi na wafanyakazi 20,000 wa Kiafrika.

Wengi wao walikuwa wakitoka mataifa ya Msumbiji, Angola, Guinea-Bissau, Cape Verde na Ethiopia. Adelino Massuvira Joao kutoka Msumbiji alikuwa na umri wa miaka 28 na akifanya kazi kwenye taasisi iliyohusika na michezo katika mji wa Suhl, ambaye anasema kwa kuanguka Ukuta wa Berlin, naye alipoteza ajira yake.

"Kampuni ikavunja mikataba yetu nasi tukajikuta mitaani hatuna kazi. Na jambo lililokuwa wazi kwetu sote ni kwamba sasa ulishafika wakati wa kulazimika kurejea makwetu."

Lakini haikuwa athari ya kijamii kwa waliokuwa wafanyakazi na wanafunzi wa Kiafrika ndani ya Ujerumani Mashariki tu wakati huo. Kulikuwa pia na athari za kisiasa kwenye mataifa watokeako, kama vile Msumbiji anakotokea Massuvira.

Ujerumani na Wajerumani sasa walikuwa na mengi ya kuwashughulisha wenyewe, na hivyo wakawaacha Waafrika hawa peke yao. Huko Msumbiji, serikali ilikuwa nayo imejiingiza kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe na kundi la waasi la RENAMO, hali sawa na ilivyokuwa Angola ambako kundi la UNITA lilikuwa likipambana na serikali.

Kwa hivyo yale yaliyokuwa yakisemwa kuwa watu wa Ujerumani Mashariki walikuwa wakijenga mahusiano ya kidugu na watu wa mataifa ya Afrika ilikuwa ni kauli ya kisiasa tu.

Ukweli ni kuwa huu ulikuwa uhusiano wa kiserikali, ambao GDR ilikuwa inautumia kusarifisha itikadi yake ya kisiasa: Usoshalisti.

"Kulikuwa kunaendelezwa mifumo ya kiitikadi na usambazaji wa falsafa," anakumbuka waziri wa wakati huo wa mambo ya nje wa Ujerumani Mashariki, Marcus Meckel