Ukraine yatumia kongamano la Davos kuomba silaha zaidi
23 Mei 2022Akishiriki kwa njia ya video kongamano hilo la kwanza la uchumi la dunia kuandaliwa nchini Uswisi katika muda wa zaidi ya miaka miwili baada ya kutofanyika kufuatia janga la virusi vya corona , Zelensky alitoa hotuba yake kuu na kusema kwamba mgogoro nchini Ukraine unaonesha kuwa msaada kwa nchi inayoshambuliwa ni wa thamani zaidi unapotolewa kwa haraka huku akitaja silaha, ufadhili, uungwaji mkono wa kisiasa na vikwazo dhidi ya Urusi.
Rais huyo wa Ukraine amesema kama wangepokea kwa asilimia 100 ya mahitaji yao kwa mara moja mnamo mwezi Februari, matokeo yake yangekuwa kuokolewa kwa maelfu ya maisha.
Zelensky asisitiza kuhusu hitaji la silaha
Zelensky ameongeza kuwa Ukraine inahitaji silaha zote inazoomba na sio zilizotolewa peke yake huku akisema watu 87 waliuawa mnamo Mei 17 wakati wa shambulizi la Urusi dhidi ya kambi moja ya kijeshi Kaskazini mwa Ukraine.
Huku hayo yakijiri, waziri wa ulinzi wa Marekani Lloyd Austin pia amelihutubia kongamano hilo la kiuchumi la Davos na kusema kuwa wakati mapigano yanaendelea nchini Ukraine, juhudi zao lazima ziongezeke na lazima wote wajipange kukabiliana na changamoto zilizoko mbele yao . Ameongeza kuwa vikosi vya kijeshi vya Ukraine vitahitaji msaada endelevu na Marekani imejitolea kusimama na Ukraine kwa muda mrefu.
Austin pia amesema kuwa mgogoro wa Ukraine umeuhamasisha ulimwengu huru na kwamba tangu uvamizi wa Urusi tarehe 24 Februari, zaidi ya washirika wao 40 na washirika wengine kutoka kote ulimwenguni wamejitokeza kutoa msaada muhimu wa kiusalama ili kuisaidia Ukraine kujilinda.
Wakati huo huo, meya wa Kyiv nchini Ukraine Vitali Klitschko, amewaambia viongozi wa kibiashara na serikali wanaohudhuria kongamano hilo mjini Davos kwamba taifa lake linatetea maadili ya kidemokrasia na maisha ya binadamu. Klitschko ameongeza kwamba Ukraine inahitaji silaha na msaada wa kisiasa na kiuchumi .
Mkuu wa IEA atoa wito wa kukomesha ongezeko la uwekezaji wa nishati chafu
Mbali na hayo, akizungumza kwenye jopo la nishati la kongamano hilo , mkuu wa Shirika la kimataifa la kudhibiti matumizi ya Nishati IEA Fatih Birol ameyataka mataifa na wawekezaji kutotumia uvamizi wa Urusi nchini Ukraine kama sababu ya kuongeza uwekezaji wa nishati chafuzi.
Birol amesema hatua za haraka za kushughulikia msukusuko wa sekta ya nishati kutokana na vita hivyo zinapaswa kuwa ongezeko la mafuta na gesi katika soko, lakini hii haimaanishi uwekezaji mkubwa na endelevu wa nishtai chafuzi.