Ukraine yakataa wito wa Urusi kwa Mariupol kujisalimisha
21 Machi 2022Wakati Urusi ikizidisha jaribio lake la kuishambulia Mariupol ili isalimu amri, mashambulizi yake katika maeneo mengine ya Ukraine yamekwama.
Serikali za magharibi na wachambuzi wanaona mzozo huo ukiendelea na kuwa vita vya uasi huku Urusi ikiendelea kuishambulia miji.
Katika mji mkuu wa Kyiv, mashambulizi ya makombora ya Urusi yaliharibu kituo cha maduka karibu na katikati mwa jiji na kuua watu wasiopungua wanane.
Soma pia: Makombora ya Urusi yaishambulia miji ya Ukraine
Mji uliozingirwa wa Mariupol umeshuhudia baadhi ya matukio ya kuogofya zaidi ya vita hiyo chini ya mashabulizi ya Urusi kwa zaidi ya wiki tatu sasa.
Mashambulizi yaliipiga shule ya sanaa walikojihifadhi watu karibu 400 saa chache tu baada ya Urusi kupendekeza kufungua njia mbili za kutoka mjini humo, kwa sharti kwamba watetezi wa mji huo wanaweka chini silaha, kulingana na maafisa wa Ukraine.
Maafisa wa Ukraine walikataa pendekezo la Urusi la njia salama kutoka Mariupol hata kabla ya kufika na kupita kwa muda wa mwisho uliotolewa na Urusi kwa Ukraine kutoa jibu.
Zelenskiy arudia wito wa kukutana na Putin
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky siku ya Jumapili alitoa tena wito wa mazungumzo ya moja kwa moja na mwenzake wa Urusi Vladimir Putin, lakini alisisitiza kuwa masharti ya Urusi kuhusiana na mamlaka ya mipaka na uhuru wa Ukraine hayakubaliki.
Katika mahojiano na CNN, Zelensky alisema yuko tayari kwa mazungumzo na Putin na anaamini kuwa mzozo wa Ukraine na Urusi hautaisha bila mazungumzo.
Soma pia:Rais Zelenskiy ataka mazungumzo ya kina na Moscow
Rais huyo pia amesema mzingiro wa Mariupol utaingia katika vitabu vya historia ya uwajibikaji kwa uhalifu wa kivita, na kuongeza kuwa walichokifanya wakaliaji ni ugaidi ambao utakumbukwa kwa karne nyingi zijazo.
"Na kadri watu wa Ukraine wanavyouambia ulimwengu kuhusu hilo, ndivyo tunavyopata msaada zaidi. Kadiri Urusi inavyozidi kutumia ugaidi dhidi ya Ukraine, ndivyo matokeo yatakavyokuwa mabaya zaidi kwake," alisema Zelenskiy.
Kuanguka kwa Mariupol kungeruhusu vikosi vya Urusi kusini na mashariki mwa Ukraine kuungana.
Lakini wachambuzi wa masuala ya kijeshi wa nchi za Magharibi wanasema hata kama mji huo uliozingirwa utachukuliwa, wanajeshi wanaopambana dhidi ya kizuizi kwa wakati mmoja kwa ajili ya udhibiti wanaweza kuwa wamechoka sana kuweza kusaidia kupata mafanikio ya Urusi katika nyanja nyingine.
Rais wa Marekani Joe Biden alitarajiwa kuzungumza baadaye Jumatatu na viongozi wa Ufaransa, Ujerumani, Italia na Uingereza kujadili kuhusu vita hivyo, kabla ya baadae wiki hii kuelekea Brussels na kisha Poland kwa mazungumzo ya ana kwa ana.
Soma pia: Marais Joe Biden na Xi Jinping wazungumza kuhusu Ukraine
Zelenskiy amekuwa akiiomba Marekani kumpatia ndege zaidi na mifumo ya kisasa ya ulinzi wa anga, huku wanachama wa jumuiya ya NATO wa Ulaya mashariki wamekuwa wakitafuta mifumo ya ulinzi wa makombora kutoka Marekani na Uingereza.
Zaidi ya wiki tatu tangu kuanza kwa uvamizi huo, pande hizo mbili sasa zinaonekana kujaribu kudhoofishana, wataalam wanasema, huku vikosi vya Urusi vilivyokwama vikirusha makombora ya masafa marefu katika miji na kambi za kijeshi huku vikosi vya Ukraine vikiendesha mashambulizi ya kupiga na kukimbia na kujaribu kuikatia Urusi njia za ugavi.
Chanzo: Mashirika