Ukraine kufungua njia 10 za kiutu
7 Aprili 2022Naibu Waziri Mkuu wa Ukraine, Iryna Vereshchuk amesema Alhamisi kuwa raia wataruhusiwa kuondoka kwenye mji wa Mariupol ambao umezingirwa na majeshi ya Urusi kwa kutumia magari binafsi kuelekea kwenye mji wa Zaporizhzhya.
Amesema mabasi ya kuelekea Zaporizhzhya yatawachukua raia kutoka kwenye miji ya Berdyansk, Tokmak na Melitopol. Vereshchuk amesema njia nyingine tano za kuwaruhusu raia kuondoka zimetengwa kutoka Luhansk kwenda mji wa Bakhmut. Njia hizo zinatangazwa kila siku.
Kuleba: Ukraine inahitaji silaha zaidi
Naye Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine, Dmytro Kuleba amesema nchi yake inahitaji silaha zaidi. Kuleba ameyatoa matamshi hayo kabla ya siku ya pili ya mikutano ya mawaziri wa mambo ya kigeni wa Jumuia ya Kujihami ya NATO, mjini Brussels.
Akizungumza pamoja na Katibu Mkuu wa NATO, Jens Stoltenberg, Kuleba ametoa wito nchi yake ipatiwe ndege zaidi, mifumo ya kujilinda na makombora, makombora na magari ya kivita kutoka kwa washirika wake wa NATO.
"Tunajua jinsi ya kupigana, tunajua jinsi ya kushinda. Ajenda yangu ni rahisi sana. Ina vipengele vitatu tu; silaha, silaha na silaha. Tuna imani kuwa njia bora ya kuisaidia Ukraine sasa ni kuipatia kila kitu kinachohitajika ili kumdhibiti Putin na kulishinda jeshi la Urusi nchini Ukraine," alisisitiza Kuleba.
Kwa upande wake Stoltenberg amesema ni muda muafaka kwa muungano huo wa kijeshi kuipatia silaha Ukraine, ikiwemo silaha za kivita.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Annalena Baerbock amesema katika majadiliano ya NATO Alhamisi kwamba muungano huo wa kijeshi unapanga kuongeza msaada kwa Ukraine ikiwepo silaha tofauti za kijeshi.
Ukraine yaishutumu Hungary kuisaidia Urusi kwenye vita
Aidha, wizara ya mambo ya nje ya Ukraine leo imeishutumu Hungary kwa kumsaidia Rais wa Urusi, Vladmir Putin katika vita vya Ukraine. Hayo yameelezwa kutokana na mazungumzo yaliyofanyika kwa njia ya simu kati ya viongozi wa Hungary na Urusi. Ukraine pia imeishutumu Hungary kwa kuvuruga umoja ndani ya nchi za Umoja wa Ulaya.
Wakati huo huo, Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky Ijumaa anatarajiwa kufanya mazungumzo na Rais wa Halmashauri Kuu ya Ulaya, Ursula von der Leyen mjini Kiev.
Msemaji wa rais wa Ukraine, Sergii Nykyforov amesema kuwa taarifa zaidi kuhusu mkutano huo hazitotangazwa kutokana na sababu za kiusalama. Msemaji wa Umoja wa Ulaya alisema siku ya Jumanne kwamba mkuu wa sera za kigeni wa umoja huo, Josep Borell pia ataizuru Kiev wiki hii.
Ama kwa upande mwingine, Borell amesema awamu mpya ya vikwazo vya Umoja wa Ulaya kwa Urusi ikiwemo marufuku ya mauzo ya mkaa, huenda ikakubaliwa ifikapo Ijumaa. Akizungumza na waandishi habari, Borell amesema umoja huo utajadiliana kuhusu vikwazo vya mafuta dhidi ya Urusi ifikapo siku ya Jumatatu.
Umoja wa Mataifa kupiga kura kuisimaisha uanachama Urusi
Huku hayo yakijiri, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa linatarajia kupiga kura iwapo iisimamishe Urusi uanachama katika Baraza la Haki za Binaadamu la umoja huo.
Kura hiyo imependekezwa na Marekani kutokana na madai kwamba wanajeshi wa Urusi waliwaua raia wakati wakiondoka kwenye mji wa Bucha, ulio karibu na mji mkuu, Kiev.
Msemaji wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Paulina Kubiak amesema kikao maalum kuhusu Ukraine kitafanyika Alhamisi na azimio hilo litapigiwa kura. Ili Urusi iweze kusimamishwa uanachama, panahitajika theluthi mbili ya kura zote bila kujumuisha wajumbe ambao watajizuia kupiga kura.
Wajumbe wa Baraza la Haki za Binaadamu lenye wanachama 47 wanachaguliwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwa vipindi tofauti vya miaka mitatu. Muhula wa Shirikisho la Urusi unamalazikika mwaka 2023, kama ilivyo kwa Ukraine.
(AFP, DPA, AP, Reuters, DW)