Ukraine imeishambulia Urusi kwa ndege zisizo na rubani
30 Agosti 2023Vikosi vya Urusi vilijibu mashambulizi ya Kyiv katika kile maafisa wa Ukraine walitaja kama "shambulio kubwa, la pamoja" ambalo liliua watu wawili.
Shirika la habari la serikali ya Urusi Tass limeripoti kwamba ndege zisizo na rubani zilishambulia uwanja wa ndege katika eneo la Pskov magharibi mwa Urusi karibu na mpaka wa Estonia na Latvia, na kuharibu njia nne za usafiri wa ndege zinayoweza kubeba mashine nzito.
Soma pia: Urusi yadungua droni mbili zilizolenga Moscow
Inaarifiwa kuwa mashambulizi katika uwanja wa ndege yaliripotiwa kwa mara ya kwanza dakika chache kabla ya saa sita usiku, na kufuatiwa na makombora makali. Ripoti za vyombo vya habari ambazo hazijathibitishwa zilisema takriban ndege 20 zisizo na rubani ziliulenga uwanja huo wa ndege.
Akizungumza na waandishi wa habari gavana wa mkoa wa Pskov nchini Urusi, Mikhail Vedernikov, amesema "Shambulio la ndege zisizo na rubani lilizuiwa. Hakuna majeruhi, asante Mungu. Upeo wa uharibifu sasa unajulikana. Huduma zote sasa zinaendelea. Na tumefanya mkutano wa dharura wa wafanyakazi, kuweka wazi hatua za msingi zitakazofuata."
Kamanda Mkuu wa Vikosi vya kijeshi vya Ukraine Jenerali Valeriy Zaluzhnyi, amesema wanajeshi wa anga wa Ukraine walidungua makombora 28 pamoja na ndege 15 kati ya 16 zisizo na rubani katika shambulio la hilo la usiku, ambalo pia lililenga eneo la Bahari Nyeusi la Odesa.
Urusi imejibu mashambulizi
Urusi kwa upande wake imesema ndege zisizo na rubani za Ukraine zilijaribu kushambulia mnara wa kituo cha televisheni katika mkoa wa Bryansk lakini hakuna majeruhi walioripotiwa na kwamba ndege zake zilidungua boti nne za kasi za Ukraine katika Bahari Nyeusi.
Huku haya yakijiri Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken alitangaza jana Jumanne mpango mpya wa msaada wa kijeshi kuisaidia Ukraine katika mapambano yake dhidi ya Urusi.
Soma pia: Urusi na Ukraine zaendelea kushambuliana kwa kutumia droni
Katika taarifa yake Blinken amesema kifurushi hicho kipya kinajumuisha vifaa vya ziada vya kusafisha migodi, makombora kwa ulinzi wa anga, pamoja na risasi za silaha na silaha ndogo.
Aidha Mawaziri wa ulinzi wa Umoja wa Ulaya wanakutana mjini Toledo, Uhispania leo Jumatano katika kiwanda cha zamani cha kutengeneza silaha, ambacho sasa ni chuo kikuu, kuzingatia msaada wa kifedha wa muda mrefu kwa Ukraine.
Hata hivyo Washirika wa Ukraine wa Magharibi kwa ujumla wanaikataza Kyiv kutumia silaha inazowasambazia katika kuishambulia Urusi lakini wanasema Kyiv ina haki ya kufanya mashambulizi kwa kutumia silaha zake.