Ujumbe wa Syria watoka nje ya mkutano wa Geneva
28 Februari 2012Wawakilishi wa Syria wamewashutumu baadhi ya wajumbe kwa kutaka kutumia jukwaa hilo na kulibadilisha kuwa la kuushambulia na kuutusi utawala wa Syria.
Balozi wa Syria katika umoja wa mataifa mjini Geneva Faysal Khabbaz , amesema kabla ya kutoka katika chumba cha majadiliano ambako mawaziri wa serikali na maafisa wa ngazi ya juu wamekusanyika kwa ajili ya mkutano huo ulioitishwa maalum na baraza la umoja wa mataifa la haki za binadamu mjini Geneva, kuwa hatua muhimu ya kuwasaidia watu wa Syria ni kuacha mara moja kuchochea mzozo wa kimadhehebu na kuacha kuwapa silaha na fedha waasi.
Khabbaz amesema kuwa mjadala huo unakiuka kabisa kanuni na kudokeza kuwa hali ya haki za binadamu nchini Syria tayari imo katika ajenda kwa ajili ya majadiliano katika kikao cha baadaye, kikao ambacho kitaendelea hadi Machi 23.
Tunaimani kuwa lengo kuu ni kuficha ukweli wa ghasia na mauaji yanayofanywa na makundi yenye silaha dhidi ya raia wasio na hatia , amesema Khabbaz.
Tangu Februari 9, hospitali 18, zahanati 48 na magari 129 ya kubebea wagonjwa yameshambuliwa na makundi ya watu wenye silaha , na imelalamika kuwa vikwazo vilivyowekwa na baadhi ya nchi vinazuwia serikali ya Syria kuweza kununua madawa na mafuta.
Ufaransa imesema kuwa baraza la usalama la umoja wa mataifa litaanza kufanyia kazi pendekezo la azimio litakalowezesha kumaliza ghasia nchini Syria na kuwezesha kupatikana njia ya kuwafikia wahanga katika ghasia hizo.
Msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni ya Ufaransa Bernard Valero amewaambia waandishi habari kuwa mchakato wa kupatikana azimio hilo katika baraza la usalama umeanza leo, na kuongeza kuwa mtazamo uko katika maeneo yaliyozingirwa ya mjini wa Homs.
Amesema kuwa matumaini ni kuwa Urusi na China hazitapinga pendekezo hilo la azimio. Kutokana na hali hiyo ya dharura , muda umewadia sasa kwa wajumbe wote wa baraza hilo , bila mtengano, kuzuwia unyama huu.
Wakati huo huo rais wa Tunisia Mancef Marzouki amesema amesema katika mahojiano ambayo yatachapishwa kesho Jumatano, kuwa nchi yake iko tayari kumpa hifadhi ya kisiasa kiongozi wa Syria Bashar al-Assad kama sehemu ya suluhisho katika mzozo wa nchi hiyo.
Mwandishi : Sekione Kitojo / afpe/rtre
Mhariri: Yusuf , Saumu.