Ujumbe wa Israel wawasili Cairo kwa majadiliano kuhusu Gaza
25 Agosti 2024Kundi la Hamas pia limetuma wawakilishi mjini Cairo, wakiongozwa na afisa wa juu Khalil al-Haya. Kama ilivyokuwa kabla, Hamas haitaki kushiriki mazungumzo hayo, lakini inataka kufahamishwa kuhusu maendeleo yake.
Sawa na ilivyokuwa katika duru ya karibuni zaidi nchini Qatar, lengo la mazungumzo ya sasa ni kuziba mianya katika misimamo ya Hamas na Israel na kufikia makubaliano juu ya kusitisha vita.
Kwa kuwa Hamas na Israel hazijadiliani moja kwa moja, Marekani, Qatar na Misri zinafanya kazi ya upatanishi.
Soma pia:Wajumbe wa Hamas wako Cairo wakati hali ya kibinaadamu ikizidi kuwa mbaya Gaza
Mfalme Tamim bin Hamad Athani, amekwenda Misri kuiwakilisha Qatar, huku mkurugenzi wa shirika la upelelezi la Marekani, CIA, William Burns, na mratibu wa taifa wa masuala ya Mashariki ya Kati Brett McGurk wakishiriki kwa niaba ya Marerkani.
Wakuu wa mashirika ya ujasusi wa ndani na nje wa Israel, David Barnea na Ronen Bar pia wamekwenda Cairo.
Mazungumzo kuhusu Gaza yanahusishwa na matumaini ya kuzuwia kutanuka zaidi kwa vita katika Mashariki ya Kati. Israel na Hezbollah, ambayo ni mshirika wa Hamas, zimekabiliana leo, katika mmoja ya mashambulizi makali zaidi katika miezi kadhaa.