Ujerumani yayakaribisha matokeo ya uchaguzi wa Ugiriki
18 Juni 2012Waziri wa Mambo ya Nje ya Ujerumani, Guido Westerwelle, ameyaita matokeo hayo ya uchaguzi wa Bunge nchini Ugiriki kama uamuzi usio wa kushangaza, lakini ambao ulikuwa muhimu sana kwa nchi hiyo iliyozama kwenye dimbwi la madeni.
Westerwelle amesema ni muhimu kwa Ugiriki kuendelea na mageuzi ya kiuchumi, kubakia kwenye sarafu ya euro, na kuamua kuendelea kuwa sehemu ya Ulaya.
Hata hivyo, linapokuja suala la mkataba wa makubaliano ya upunguzaji wa deni la Ugiriki uliofungwa baina ya nchi hiyo na Umoja wa Ulaya, Westerwelle amesema hakutakuwa na mabadiliko. “Lakini hili libakie kuwa wazi kabisa, kwamba mkataba si wa kujadiliwa tena na utabakia kama ulivyo.”
Hii ni kinyume na ahadi ya vyama vya New Democracy na PASOK vinavyotarajiwa kuunda serikali ya mseto ya Ugiriki. Vyama hivyo vilisema kwamba vitahakikisha mkataba huo unajadiliwa upya na makubaliano mapya yanafikiwa.
Merkel asema hakuna kitakachobadilika kwenye mkataba
Kauli ya Westerwelle ni sawa na ya Kansela Angela Merkel, ambaye katika hafla iliyoandaliwa na chama chake cha CDU huko Hesse siku ya Jumamosi, alisema kwamba makubaliano hayo yanapaswa kwenda kama yalivyokwishapitishwa na si kinyume chake.
Serikali ya Ujerumani, kwa ujumla wale, inaipokea serikali mpya ya Ugiriki kwa mikono miwili, hasa baada ya kwamba imekuja muda mkwamo wa muda mrefu wa kisiasa, ukweli ambao Westerwelle anasema una maana kubwa sana kwa kile kinachoweza kuja hapo baadaye katika mataifa mengine ya Ulaya.
“Ikiwa tutawaambia Wagiriki kuwa ni sawa mulivyoamua na haidhuru muda mrefu muliochukua kufikia maamuzi hayo, hilo litakuwa tatizo kwa nchi nyengine za Ulaya, ambazo zina moyo na zimejitolea kutekeleza sera za mageuzi.” Amesema Westerwelle.
Wajibu wa Ugiriki si kwa Wagiriki tu
Akitathmini kipindi kirefu kilichochukuliwa na wanasiasa wa Ugiriki kabla ya uchaguzi wa jana, kiongozi wa chama cha SPD, Sigmar Gabriel, amesema kile anachotarajia ni kuwa na serikali imara, ambayo haitachukulia yaliyomo kwenye mkataba wa Umoja wa Ulaya mtaji wake wa kisiasa.
Kauli mfano wa hiyo imetolewa pia na naibu mwenyekiti wa muungano wa CDU/CSU katika bunge la Ujerumani, Michael Meister. “Yeyote ambaye anaunda serikali mpya ya Ugiriki, suala ni ikiwa atayaheshimuje makubaliano ya kupokea fedha kutoka Umoja wa Ulaya. Na ikiwa hawawezi kuyaheshimu, nina shaka kama wataweza kusalia kwenye sarafu ya euro."
Kwa upande wake, Rais wa Bunge la Ulaya, Martin Schulz, amesema anaamini kwamba Ugiriki itasonga mbele kutekeleza mpango mzima wa kubana matumizi. Shulz, mwanasiasa kutoka chama cha SPD cha Ujerumani, amesema serikali inayoingia kwenye mkataba unaojumuisha hatima ya mataifa mengine, lazima iwajibike kwa raia wake na kwa raia wa washirika wake.
Mwandishi: Sabine Kinkartz/DW Berlin
Tafsiri: Mohammed Khelef
Mhariri: Othman Miraji