Ujerumani yawakamata raia watatu kwa kuifanyia China ujasusi
22 Aprili 2024Waendesha mashitaka wa Ujerumani wamewakamata watu watatu raia wa Ujerumani kwa tuhuma za kufanya ujasusi kwa ajili ya idara ya usalama ya China.
Kwa mujibu wa ofisi ya mwendesha mashitaka ya shirikisho ya Ujerumani, watuhumiwa hao, wanaume wawili na mwanamke mmoja walikamatwa kwenye miji ya magharibi ya Dusseldorf na Bad Homburg siku ya Jumatatu.
Fuatilia habari hii:Ujerumani, China zafanya mazungumzo ya ngazi ya juu
Wanashukiwa kuwa walikuwa wakifanya kazi na idara ya usalama ya China tangu Juni mwaka 2022 na wamekiuka sheria ya biashara ya kimataifa na malipo katika muktadha huo.
Kesi hiyo inahusu utoaji wa taarifa za teknolojia ya kijeshi kwa idara ya usalama ya China. Wakati wa kukamatwa kwao, washukiwa hao walikuwa kwenye mazungumzo kuhusu miradi ya utafiti ambayo inaweza kuwa na manufaa kwa upanuzi wa nguvu za kijeshi za baharini za China, kulingana na waendesha mashtaka.
Soma: Ujerumani yazindua mkakati mpya wa kuamiliana na China
Mmoja wa washukiwa hao anasemekana kuuza taarifa za teknolojia ya ubunifu wa kijeshi kwa mfanyakazi wa idara ya usalama ya China MSS.
Washukiwa hao watafikishwa mbele ya hakimu wa Mahakama ya Shirikisho siku ya Jumatatu na Jumanne.