1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yafuzu duru ya mtoano kombe la EURO

Josephat Charo
20 Juni 2024

Wenyeji Ujerumani imekuwa timu ya kwanza kufuzu kwa duru ya mtoano baada ya kuichapa Hungary 2-0 kupitia mabao ya Jamal Musiala na nahoha Ilkay Gundogan.

https://p.dw.com/p/4hHEE
Nahodha wa Ujerumani Ilkay Gundogan akitia kambani bao dhidi ya Hungary
Nahodha wa Ujerumani Ilkay Gundogan akitia kambani bao dhidi ya HungaryPicha: Leonhard Simon/REUTERS

Jamal Musiala alionyesha umahiri wake na kuwathibitishia wachezaji wenzake wanaofikiri mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 21 anaweza kufika mbali na kuwa miongoni mwa wachezji bora wa soka duniani. Musiala alitia kambani bao lake la pili kwenye mashindano hayo kuisadia Ujerumani kupata ushindi huo na kujikatia tiketi ya kusonga mbele.

Kocha wa Ujerumani Julian Nagelsmann amesema mashabiki sasa wanaweza kuota ndoto ya kwenda Berlin kushudia fainali. Amesema ana furaha ingawa haikuwa mechi nyepesi dhidi ya wapinzani wagumu. Mianya ilizibwa kabisa lakini wakafanikiwa kupata upenyo na kufunga mabao baada ya kuonesha uvumilivu.

Kocha Nagelsmann amesema Jamal Musiala alicheza vizuri katika mechi zote mbili, sio tu kwa kufunga mabao mawili bali katika kila hali, au ushambuliaji, ni vigumu sana kwa beki kumzuia. Nagelsmann amesema Musiala anatakiwa tu aelekeze nguvu katika uwezo wake wa kutandaza kandanda na asifikirie shinikizo linalomkabili.

Mchezaji bora wa mechi na nahodha wa timu ya Ujerumani Ilkay Gundogan amesema kwake yeye ni jambo jema kucheza na Musiala, kwa kuwa ana uwezo wa kufanya jambo lisilotarajiwa katika kila hali na pengine ni mchezaji muhimu zaidi kwao wao kwa wakati huu, akiwa angali na umri mdogo pia.

Nahodha wa Ujerumani Ilkay Gundogan akifunga bao dhidi ya Hungary
Nahodha wa Ujerumani Ilkay Gundogan akifunga bao dhidi ya HungaryPicha: Heiko Becker/REUTERS

Scotland wafufua matumaini yao

Katika mechi nyingine ya kundi A, Scotland imejizatiti kuyaweka matumaini yao hai kuendelea kucheze katika mashindano ya EURO baada ya kutoka sare 1-1 na Uswisi. Uswisi imepoteza fursa nzuri ya kusonga mbele duru ya mtoano ya timu 16 bora wakiwa na mechi moja mkononi.

Hungary sasa inakabiliwa na kibarua kigumu ikitarajia kucheza mechi yake ya mwisho ya kundi A dhidi ya Scotland Jumapili ijayo, huku Ujerumani wao wakiwa na miadi na Uswisi.

Sare ya kati ya Croatia na Albania na hali katika kundi C ina maana kutakuwa na angalau washindi bora wa nafasi ya tatu ambao hawatafikia alama sita za Ujerumani. Timu nne bora zitakazokamilisha katika nafasi ya tatu katika makundi yote sita, zitafuzu kwa duru ya mtoano pamoja na timu mbili bora zitakazokamilisha katika nafasi ya kwanza na ya pili katika kila kundi.

Fainali ndogo kati ya Italia na Uhispania

Leo jioni Slovenia itakwaana na Serbia huku Denmark ikiwa na miadi na England katika mechi za kundi C. Baadaye mabingwa watetezi wa kombe la EURO Italia watanyukana na Uhispania katika pambano la kundi B. Kocha wa Uhispania Luis de la Fuente anaiona mbungi hiyo kuwa muhimu zaidi hadi sasa na ni mechi ya maamuzi na fainali ya mapema.

Mashabiki wa Sctoland wakiishangilia timu yao
Mashabiki wa Sctoland wakiishangilia timu yaoPicha: Matthias Schrader/AP/picture alliance

Kocha huyo amesema timu hizo zina mambo mengi yanayofanana kwa hiyo utakuwa mchezo mgumu wa kiwango cha juu ambao wnausubiri kwa hamu kubwa. Amesema ataamua kama akifanyie mabadiliko kikosi chake cha kwanza baada ya ushindi mnono wa 3-0 dhidi ya Croatia, lakini akawahimiza wachezaji wake waendelee kuboresha mchezo wao, akisema safari ni ndefu kama mbio za nyika na wanafahamu fika uwezo wa timu nyingine kama vile Ufaransa, Ujerumani, England na Italia.

Italia na Uhispania zinashuka dimbani kwa mechi ya pili ya makundi zikiwa na alama tatu kibindoni baada ya kushinda mechi zao za ufunguzi na mshindi wa kipute cha leo atajihakikishia nafasi ya kusonga mbele katika duru ya mtoano ya timu 16 bora.

Serbia na Albania zatozwa faini

Kwingineko shirikisho la soka barani Ulaya, EUFA limeyatoza faini ya euro 10,000 mashirikisho ya soka ya Serbia na Albania kila moja baada ya mashabiki wao kusambaza ujumbe wa uchokozi usiofaa kwa mashindano ya michezo. Shirikisho la UEFA limesema hayo jana Jumatano bila kutoa maelezo zaidi.

Soma pia: Conceicao aipa ushindi Ureno dakika za mwisho

Vyombo vya habari vya Uingereza viliripoti kwamba kelele za tumbiri zilitolewa kuwaelekea wachezaji wa England wakati wa mechi ya kwanza ya makundi dhidi ya Serbia mjini Gelsenkirchen Jumapili iliyopita. Shabiki hakukamatwa wala kufukuzwa atoke uwanjani wakati wa mechi hiyo ambayo England ilishinda 1-0, ingawa wasimamizi wa uwanja na maafisa wa polisi walikuwepo wakishuhudia.

Shirikisho la soka la Serbia pia litalazimika kulipa faini ya euro 4,500 kwa sababu ya vitu vilivyorushwa kutoka kwenye maeneo wanakokaa mashabiki. Shirikisho la soka la Albania lilitozwa faini inayofikia jumla ya euro 27,375 kwa mashabiki wao kuwasha fashifashi, kurusha vitu na kuvamia uwanja katika mechi waliyoshindwa na Italia 2-1 Jumamosi iliyopita.

(ap, dpa)