1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yaunga mkono upelekaji misaada zaidi Gaza

Hawa Bihoga
30 Aprili 2024

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Annalena Baerbock, ameunga mkono misaada zaidi ya kibinaadamu kupelekwa katika eneo la Ukanda wa Gaza na suluhisho la mataifa mawili.

https://p.dw.com/p/4fLgi
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Annalenna Baerbock.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Annalenna Baerbock.Picha: Kira Hofmann/AA/photothek.de/picture alliance

Katika mazungumzo na mawaziri wenzake wa nchi za Magharibi na Kiarabu mjini Riyadh, Saudi Arabia, Baerbock alisema uhuru wa taifa la Palestina ni sehemu ya mchakato wa amani na suluhisho la serikali mbili bado ni lengo dhahiri la serikali ya Ujerumani.

Israel inalikataa pendekezo hilo na kundi la Hamas linataka dola la Palestina bila kuitambua Israel.

Soma zaidi: Israel yaendeleza mashambulizi katika ukanda wa Gaza

Akizungumzia misimamo hiyo, Waziri wa Mambo wa Nje wa Saudi Arabia, Faisal bin Farhan, alisema kuendelea kwa mpango wa kijeshi na kuzuiwa kwa suluhisho la serikali mbili "hakutamnufaisha yeyote zaidi ya wale wenye msimamo mkali wa pande zote na, bila shaka, kutaendelea kuyumbisha usalama wa eneo hili."

Bearbock alishiriki katika mkutano huo uliokuwa umeandaliwa kwa ushirikiano wa Saudi Arabia na Norway, ambao miongoni mwa ajenda zake ilikuwa ni suluhisho la mataifa mawili na kutambuliwa kwa Palestina.