Ujerumani yataka mzozo wa Gaza umalizike
5 Septemba 2024Akizungumza Alhamisi mjini Riyadh na mwenyeji wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia, Faisal bin Farhan Al-Saud, Baerbock amesema mpango wa kusitisha mapigano uliopendekezwa na Rais wa Marekani, Joe Biden mwezi Mei, unapaswa kupitishwa. Wizara ya mambo ya nje ya Ujerumani hapo awali ilisema kuwa Baerbock na Al-Saud pia watajadiliana kuhusu mashambulizi katika meli za kimataifa yanayofanywa na waasi wa Kihouthi wa Yemen ambao wanaungwa mkono na Iran.
Ziara ya Baerbock Mashariki ya Kati itampeleka Jordan na Israel
Baadae Alhamisi, mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya njuu wa Ujerumani ataelekea Jordan, kwa mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo, Ayman Safadi, mjini Amman. Mazungumzo yao yataangazia zaidi juhudi za kiutu katika Ukanda wa Gaza, kwani Jordan ni mshirika mkuu wa nchi na mashirika ya kutoa misaada yanayofanya kazi ya kupeleka misaada kwenye ardhi ya Palestina ambayo imezingirwa.
Siku ya Ijumaa, Baerbock ataelekea Israel ambako atafanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel, Israel Katz, na Waziri wa Ulinzi Yoav Gallant. Baada ya hapo ataelekea Ramallah, katika Ukingo wa Magharibi, na atakutana kwa mazungumzo na Waziri Mkuu wa Mamlaka ya Palestina, Mohammed Mustafa.
Huku hayo yakiarifiwa, mkuu wa jeshi la Misri, Luteni Jenerali Ahmed Fathy Khalifa leo amefanya ziara ambayo haikupangwa katika mpaka wa nchi hiyo na Ukanda wa Gaza, kukagua hali ya usalama. Video iliyochapishwa na jeshi imemuonyesha Luteni Jenerali Khalifa akizungumza na wanajeshi katika eneo la kuvukia katika upande wa Misri la Rafah, ambapo alisikiliza maoni na maswali ya wanajeshi hao. Kamanda huyo wa jeshi amesisitiza kuwa jukumu kubwa la vikosi vya jeshi ni kulinda mipaka ya nchi.
Netanyahu: Israel kutoacha kudhibiti Ushoroba wa Philadelphi
Ziara hiyo inafanyika baada ya Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu jana Jumatano kusema kuwa Israel haitoacha kudhibiti Ushoroba wa Philadelphi, na itakubali tu makubaliano ya kudumu ya kusitisha mapigano, ambayo yatahakikisha kwamba njia inayoitwa "Ushoroba wa Philadelphi," iliyopo katika eneo la mpaka kati ya kusini mwa Gaza na Misri haiwezi kamwe kutumika kama njia inayotumiwa na kundi la Hamas. Ujia huo umekuwa moja ya vikwazo vikubwa katika mpango wa kusitisha mapigano Gaza na kuwaachia mateka wa Israel wanaoshikiliwa na Hamas, kwa kubadilishana na wafungwa wa Kipalestina.
Wakati huo huo, Umoja wa Mataifa umeanza awamu ya pili ya kutoa chanjo ya polio kusini mwa Gaza, kwenye maeneo ya Rafah na Khan Younis. Wapalestina walikusanyika Alhamisi katika vituo vya afya kuwapeleka watoto wao kupata chanjo. Shirika la Umoja wa Mataifa linalotoa misaada kwa Wapalestina, UNRWA limesema kuwa hadi sasa watoto 187,000 wameshachomwa chanjo ya polio.
(AFP, DPA, AP, Reuters)